Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira yaipongeza SIDO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imelipongeza Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kuendesha Mfuko wa Taifa Kuendeleza Wajasiliamali Wananchi (NEDF) kwa mafanikio na kulitaka Shirika hilo kuongeza ubunifu katika kutafuta njia mbalimbali za kutunisha mtaji wa Mfuko huo ili kuwawezesha wananchi wengi mijini na vijijini kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) wakati wa utoaji wa Taarifa ya utekelezaji wa Mfuko (NEDF) kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Februari 5, 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo na walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha Mfuko wa NEDF hususani katika kutafuta njia za kuongeza fedha za mtaji wa Mfuko, utoaji wa mikopo mijini na vijijini kwa kuzingatia makundi maalumu, muundo wa uendeshaji, viwango vya mikopo, vigezo vya kupata mikopo, riba ya mikopo hiyo na ufadhili wa vikundi vya wajasiliamali.

Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) aliihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha SIDO inawezeshwa na inaongezewa mtaji katika Mfuko wa NEDF ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.

Naye, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alisema ni muhimu kuiwezesha SIDO kuongeza mtaji katika Mfuko huo wa NEDF kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo kishirikiana na taasisi za umma ili Mfuko huo uweze kusaidia wananchi wengi wanaohitaji mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Awali, akitoa utoaji wa Taarifa ya utekelezaji wa Mfuko (NEDF), Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji alieleza kuwa Mfuko huo umeweza kudumu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994 na umepokea jumla ya Shilingi 6,648,886,000 katika kipindi cha mwaka 1994/1995 hadi 2020/2021 kama mtaji na kuukuza hadi kufikia Shilingi 9,765,670,054.

Aidha, Prof. Mpanduji amesema huduma za kifedha za Mfuko wa NEDF zimeendelea kutolewa katika mikoa yote na inajipanga kutoa huduma hiyo katika kila wilaya huku ikitafuta njia bora za kuimarisha mfuko na kukusanya madeni sugu ya mikopo iliyotolewa.