Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira yaishauri SIDO kuwasaidia Wajasiriamali


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira yaishauri Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuwasaidia Wajasiriamali hasa katika upatikanaji wa teknolojia rahisi, mikopo yenye riba nafuu na  kuongeza uzalishaji wa mashine.

Hayo yamesemwa tarehe 24 Januari, 2023 na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) katika kikao cha kupokea taarifa ya Utendaji na Utekelezaji wa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Kihenzile amesema kuwa SIDO inapaswa kushirikiana kwa karibu na vituo vya kutoa teknolojia ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa walioko vijijini ili kuchangia upatikanaji wa ajira. 

Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) aliishukuru kamati hiyo kwa michango yao mizuri na kuahidi kutekeleza maelekezo yote ya kamati yaliyotolewa kwa lengo la kuleta tija kwenye sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara nchini.

Mhe. Kigahe amesema kuwa SIDO imeendelea kuweka miundombinu wezeshi na saidizi kwa ajili ya Wajasiliamali nchini kwa kuwaweka eneo moja na kuwasaidia teknolojia, mashine, vifungashio na kupatiwa mikopo.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo wakichangia kwa nyakati tofauti wametoa maoni na mapendekezo mbalimbali wakiitaka wizara kupitia SIDO kuongeza jitihada zaidi ya kuwasaidia Wajasiriamali hasa katika upatikanaji wa teknolojia rahisi, upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu,  kuongeza uzalishaji wa mashine za kutosha ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi Nchini hasa walioko vijijini.

Awali akiwasilisha taaraifa ya Utekelezaji wa majukumu, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Prof. Sylivester Mpanduji amesema kuwa jukumu la msingi la SIDO ni kuratibu shughuli zote za miradi ya Viwanda vidogo nchini ikilenga utoaji wa teknolojia za kiufundi, kuendeleza ubinifu wa teknolojia na mawazo ya bidhaa mpya chini ya programu ya kiatamizi.