Habari
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YATEMBELEA KIWANDA CHA NAMELA DAR ES SALAAM

Kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti tarehe 9 Machi, 2022 imefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha nguo na mavazi cha Namela Textile Limited kilichopo Gongolamboto jijini Dar es saalam.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) pamoja Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Hamad Masauni Chande (Mb) wameambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kutembelea kiwanda cha Namela Textile Limited kilichopo Gongolamboto jijini Dar es salaam.
Kiwanda cha Namela ambacho kinachakata pamba na kupeleka kiwanda cha NIDA kilichopo Tabata jijini Dar es salaam ambapo ndio bidhaa mbalimbali huzalishwa zikiwemo khanga, Vitenge na Mashuka kimeajiri wafanyakaji wapatao 3,000 ambapo bidhaa zao wanauza ndani na nje ya nchi na masoko yao makubwa ni nchi za SADC, EAC na soko la AGOA.Kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti imeridhishwa na uzalishaji wa kiwanda hicho licha ya changamoto walinazo ambazo Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.
Daniel Sirro Baran (Mb) amesema kuwa kiwanda cha Namela na NIDA kiwanda cha mfano kwani ni miongoni mwa Viwanda vya uchakataji wa pamba ambacho kinatumia pamba inayozalishwa ndani ya nchi ambayo matumizi yake ni asilimia 30 tu ya pamba yote.
Katibu Mtendaji wa TEGAMAT nchini ndugu Adam Zuku amesema kuwa Viwanda vya uchakataji wa pamba nchini vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ushindani usio sawa kwa wazalishaji wa ndani kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Aidha ndugu Adam Zuku amesema kuwa ukwepaji wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambapo wamekuwa wakiikosesha serikali mapato, ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto ya uagizaji wa nguo kutoka nje ya nchi na mizigo ya transit ambayo imekuwa haifiki inapoenda na wamekuwa wakiichepusha na kufanya biashara nchini.
Waheshimiwa wabunge wamepongeza kazi nzuri inayofanywa na kiwanda hiki na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali yakiwemo kutangaza bidhaa zao katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na Mikoani.