Habari
KAPINGA AKUTANA NA SBL KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KUKUZA VIWANDA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amekutana na kuzungumza na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ikiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha Bw. Emmanuel Kyarwenda jijini Dodoma, Machi 17, 2026.
Kikao hicho Waziri Kapinga akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara ya Wizara Bw. Sempeho Manongi cha kimkakati kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuendeleza ajenda ya Tanzania ya kukuza viwanda, kuongeza thamani ya bidhaa, na kupanua fursa za kiuchumi.
Katika kikao hicho, Waziri Kapinga ameipongeza Kampuni hiyo kwa uwekezaji wake endelevu na kueleza kuwa Serikali inathamini wadau wa sekta binafsi ikiwemo Kampuni ya Bia ya Serengeti, ambao wanaendelea kuchangia maendeleo ya viwanda nchini kupitia uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, na kutengeneza ajira kwa wananchi wengi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa SBL, Bw. Emmanuel Kyarwenda, amesema Kampuni ya Bia ya Serengeti inaendelea kujizatiti na kuunga mkono safari ya Tanzania ya kukuza viwanda. Kupitia uwekezaji wake katika uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, na kuimarisha mitandao ya ugavi wa ndani, kampuni hiyo inachangia ukuaji wa uchumi huku ikifungua fursa kwa Watanzania wengi katika mnyororo wake wa thamani.
Kama mojawapo ya wazalishaji wakubwa nchini, SBL ina mchango mkubwa katika sekta ya viwanda kupitia viwanda vyake vilivyopo Moshi, Dar es Salaam na Mwanza, ambavyo vinaendelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani sambamba na kuunda ajira na fursa za kiuchumi katika sekta mbalimbali.
Kupitia shughuli zake, SBL imetoa ajira rasmi zaidi ya watu 800, huku takribani watu 140,000 wakinufaika kupitia mnyororo wake mpana wa thamani, wakiwemo wasambazaji, wasafirishaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya huduma za ukarimu na utalii.
