Habari
Kigahe Aziagiza Taasisi kuwafuata wafanyabiashara na kutoa elimu kuhusu tozo
Kigahe Aziagiza Taasisi kuwafuata wafanyabiashara na kutoa elimu kuhusu tozo
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) amezishauri Taasisi za Umma ziwafuate, zijifunze mazingira na changamoto za wafanyabiashara na kuwapa elimu kuhusu kodi, ada, na tozo mbalimbali na si kuwasubiri ofisini ili kuendelea kuweka mazingira bora ya biashara ambayo yataleta faida kwa wafanyabiashara na kuongeza mapato ya Serikali.
Kigahe ameyasema hayo Agosti 10, 2023 wakati wa ziara yake katika Mkoa wa Songwe ambapo alitembelea Kiwanda cha Kahawa cha GDM na Kiwanda cha ILASI SEMBE vilivyopo Wilaya ya Mbozi pamoja na kuongea na wafanyabishara wa Mkoa wa Songwe kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji, kusikiliza na kutatua changamoto.
Akiongea na wafanyabiashara wa Mkoa huo, Kigahe amewashauri wawe waadilifu, waaminifu, wawazi na wasioruhusu mianya ya rushwa katika ufanyaji biashara ili kurahisisha jitihada za kupunguza tozo, faini, kodi na upatikanaji wa mikopo kwa riba nafuu hali ambayo itasaidia kukuza biashara zao , kuongeza ajira na kuongeza mapato kwa Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewataka Watumishi wa Umma na Sekta binafsi hususani Taasisi za kifedha kutoa huduma kwa wafanyabiashara kwa weledi, uaminifu, uadilifu na usawa katika ugawaji wa fursa mbalimbali ikiwemo nafasi za masoko ili wafanyabiashara wajenge imani na kupata fursa za kuendeleza biashara zao kama wanavyostahili.
Awali akiongea na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi Bw. Mbwana Kambangwa Kigahe ameipongeza Halmashauri hiyo kwa hatua iliyoichukia katika kupunguza tozo na ada na kusababisha ongezeko la makusanyo ya ushuru kutoka Bilioni 3 hadi 5 kati ya 2021/22 na 2022/23 hali inayoonyesha matokeo chanya ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (MKUMBI)
Vilevile, Kigahe amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mazingira bora ya biashara ikiwemo miundombinu ya umeme, maji, barabara, masoko pamoja na urekebishaji wa Sheria na ufutaji au upunguzaji wa kodi na tozo mbalimbali ili kuwawezesha kufanya biashara kwa tija, kukua na kuweza kushindana katika soko la kimataifa.