Habari
Kigahe :Ni muhimu kuongeza Thamani Mazao ya Wakulima

Kigahe :Ni muhimu kuongeza Thamani Mazao ya Wakulima
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe (Mb.) amesema ni muhimu kuwa na Viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kusaidia kuchakata na kuongeza thamani mazao yanayolimwa nchini ikiwemo matunda kwa mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi .
Kigahe ameyasema hayo Julai 5, 2023 kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika katika Kiwanja cha John Mwakangale jijini Mbeya ambapo alikuwa Mgeni Rasmi wa siku hiyo akiwa ameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais -TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Dugange aliyekuwa mgeni rasmi mwenza .
Akiongea wakati wa majumuisho baada ya kutembelea maonesho hayo, Mhe Kigahe amesema kuwa wakulima wanatumaini kuona mazao yao yanaongezwa thamani kupitia Viwanda vilivyopo nchini Ili wauze na kupata kipato kwa ajili ya familia zao na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Vilevile, amewashauri Wakulima kutoka Kilimo cha mazoea kwenda kwenye Kilimo cha kisasa kinachotoa matokeo ya haraka ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewapongeza waandaji wa Maonesho hayo kwa kuwahusisha wakulima wengi wa chini ambao wanatakiwa kupewa kipaumbele ili waweze kutambulika na kukua
"Nimevutiwa sana na Banda la Makete ambalo linashamba darasa la bustani ya kilimo cha ngano kwa maana nchi yetu inakabiliwa na upungufu wa ngano, hivvyo ulimaji wa ngano hapa nchini utasaidia kuondoa kero ya upatikanaji wa ngano ambayo imekuwa ikiagizwa kutoka nje ya nchi" .Amesema Kigavhe
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais -TAMISEMI Mhe. Festo Dugange (Mb.) amesema kuwa Maonesho haya yanatoa fursa ya watanzania kujifunza na kubadilishana utaalamu kutoka kwa wakulima wengine ili wapate maarifa yatakayowawezesha kulima kilimo chenye tija.