Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MRADI WA UMEME KILINDI WAFIKIA ZAIDI YA ASILIMIA 35, KUKAMILIKA MWISHO WA MWAKA


Serikali imeeleza kuwa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kilindi umefikia asilimia 35.9, huku ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ukiwa umefikia asilimia 30.91 hadi kufikia Januari 2026, na miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo Januari 30, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Mhe. Salehe Mhando, kwa niaba ya Waziri wa Nishati.

Katika swali lake, Mbunge Mhando amehoji mpango wa Serikali wa kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika jimbo la Kilindi.

Akijibu, Waziri Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuboresha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Kilindi, ikiwemo ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kilindi pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya kilovolti 132 kutoka Mkata hadi Kilindi.

Ameongeza kuwa, sambamba na miradi hiyo, TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya umeme iliyochakaa pamoja na kubadilisha nguzo za miti kwa kuweka nguzo za zege, hatua inayolenga kupunguza kukatika kwa umeme kunakotokana na kudondoka kwa nguzo za miti wakati wa mvua au matukio ya kuchomwa moto.