Habari
Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya latoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya limetoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili kujadili njia sahihi za kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini katika sekta za kiuchumi ikiwemo Kilimo, Utalii, Nishati, Madini, Tehama, Usafirishaji na Ujenzi na fursa zilizopo katika nchi 27 za Umoja wa Ulaya.
Waziri Kijaji ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya linalofanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2023 JNICC, Dar es Salaam likijumisha zaidi ya zaidi ya 800 kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania.
Aidha Dkt. Kijaji amesema katika Kongamano hilo Hati za makubaliano tatu zimetiwa saini ambapo Hati ya kwanza ilijumuisha Hati ya Makubaliano ya Huduma ya Usafiri wa Anga iliyotiwa saini na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Mbalawa na Waziri wa Mambo ya nje, Biashara na Vivutio vya Uchumi wa Ufaransa Olivier Becht ambapo makubaliano hayo yatawezesha kuongeza idadi ya safari za ndege kati ya Tanzania na Ufaransa ikiwemo safari za moja kwa moja kutoka Dar es salaam kwenda ufaransa ifikapo Juni 2023
Aidha, Hati ya makubaliano ya pili iiliyohusu ujenzi wa Mradi wa uzalishaji wa umeme wa Kakono Hydro Power utakaojengwa Mkoani Kagera unaofadhiliwa na Benki ya Maendelleo ya Afrika chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Hati ya tatu ya makubaliano ni kati ya Bandari ya Antwerp-Bruges International na Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA ambapo Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mboso amesema makubaliano hayo yataongeza ufanisi katika shughuli za bandari na kuzidi kukuza uchumi wa nchi kutokana na mapato yatakayo kusanywa na bandari hiyo.
Naye Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB), Thomas Östros, amesema Benki hiyo ya EIB imerudi nchini baada ya UVICO- 19 na iko tayari kufanya uwekezaji mkubwa wenye thamani ya EUR milioni 540 kwa kuwawezesha wawekezaji na wafanyabiashara nchini wakiwemo wanawake, na kampuni zinazojihusisha na uchumi wa Blue.