Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

LONDO - TBS NDIYO NGUZO KUU YA KULINDA AFYA ZA WALAJI


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) amelitaja Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa ni nguzo kuu ya kulinda afya za walaji na kuchochea ustawi wa viwanda nchini.

Amebainisha hayo wakati wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika hilo pamoja na Utoaji wa Tuzo kwa watumishi wa sasa na wastaafu kwa kutambua mchango wao uliojenga misingi imara ya udhibiti wa ubora Juni 6,2026, Jijini Dar es Salam.

Mhe.Londo amebainisha kuwa Kutokana na kukua kwa kasi kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali kuna uhitaji wa mifumo thabiti ya uhakiki wa ubora ili kulinda soko la ndani hivyo TBS Kupitia huduma zake imekuwa chachu ya kukuza viwanda vya ndani na kuongeza imani ya walaji, jambo linalonufaisha Tanzania katika fursa za masoko makubwa ikiwemo Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Aidha amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza uchumi kupitia maboresho ya miundombinu ya usafirishaji, nishati, na mifumo ya kidijitali na ameeleza kuwa maboresho ya sera na sheria yanalenga kuvutia uwekezaji na kuimarisha sekta binafsi, huku akiiasa TBS kuhakikisha kuwa ongezeko la uzalishaji nchini linaenda sambamba na uzingatiaji wa viwango vinavyotambulika duniani.

Mhe. Londo pia amelitaka Shirika hilo kuwekeza kwenye maabara zenye vifaa vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi, pamoja na kuimarisha mifumo ya kidijitali yenye ufanisi ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na ubunifu duniani.

Mkakati huo wa kuimarisha mifumo ya viwango unaelezwa kuwa msingi imara wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kisasa, jumuishi, na unaotegemea uzalishaji wenye thamani kubwa na kuongeza kuwa kusimamiwa vyema kwa usalama na ubora wa bidhaa kutasababisha bidhaa na kukubalika kwa urahisi duniani

Vile vile Naibu Waziri alitoa rai kwa sekta binafsi, wazalishaji, na wafanyabiashara kuendelea kushirikiana kwa karibu na TBS ili kujenga utamaduni endelevu wa uzingatiaji viwango na uzalishaji wenye tija.