Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

LONDO AHIMIZA UWEKEZAJI WA VIWANDA KUKABILI CHANGAMOTO YA AJIRA NCHINI


Uimarishaji na uanzishaji wa viwanda nchini umetajwa kuwa ndiyo suluhisho la kudumu la kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, huku⁶ ukichochea ukuaji wa uchumi jumuishi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Umuhimu wa sekta hiyo unatajwa kuwa nguzo kuu ya kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na ushindani katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kote.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb), wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha Federal Industry Limited Machi 17, 2026 wilayani Mkuranga (mkoa wa Pwani).

Mhe. Londo, akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), amepongeza uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti uliowezesha kiwanda hicho cha polyrethane (povu la magodoro) kuanza kazi, akibainisha kuwa huu ni ushahidi tosha wa imani ya wawekezaji kwa Serikali iliyopo madarakani.

Katika hotuba yake, Londo amebainisha mambo manne muhimu yaliyopo katika mradi huo: kwanza, mchango wa ajira ambapo zaidi ya Watanzania 500 wanatarajiwa kunufaika; pili, upatikanaji wa bidhaa bora za malazi nchini; tatu, ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi; na nne, kuchochea ukuaji wa viwanda vingine katika mnyororo wa thamani wa bidhaa za povu na samani.

Aidha, amesisitiza kuwa mradi huo wenye ukubwa wa hekari 120 ni kitovu kipya cha fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Mkuranga na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia changamoto za miundombinu, Mhe. Londo amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Mamlaka za Serikali za Mitaa itashughulikia uboreshaji wa barabara inayoelekea kiwandani hapo ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa. Amesema kuwa miundombinu bora ni kipaumbele cha Serikali katika kuhakikisha shughuli za uzalishaji hazikwami na gharama za kufanya biashara zinapungua.

Hatahivyo, kuhusu ombi la msamaha wa ushuru wa malighafi (Duty Remission), Londo ameeleza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itafanya uchambuzi wa kina.