Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MAENEO MAALUM YA UZALISHAJI KWA MAUZO YA NJE YAZIDI KUONGEZEKA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa katika jitihada ya kuhakikisha lengo la kufungamanisha uzalishaji wa viwanda na Sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi linatekelezwa vizuri, sasa Tanzania ina Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje 160 yanayosaidia kuongeza kiwango cha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.

 

Prof. Mkumbo ameeleza hayo wakati akitoa salamu na taarifa ya maendeleo ya viwanda nchini katika ziara ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua kiwanda cha nyama cha Eliya Food overseas Ltd kilichopo Eurendeke Longido Mkoani Arusha leo Oktoba 18, 2021.

 

Amesema uzinduzi wa kiwanda cha Eliya Food overseas Ltd umeongeza idadi ya viwanda vya nyama kufikia 10 nchini na ndio kiwanda kikubwa kuliko vyote vya kusindika nyama na eneo la kiwanda kilichozinduliwa lipo katika eneo maalum ya uzalishaji kwa mauzo ya nje ambalo litasaidia kutupatia fedha za kigeni.

 

Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa katika jitihada za kuanzisha na kuendeleza mitaa ya viwanda mpaka sasa ipo mitaa 24 nchi nzima na katika mkoa wa Arusha ipo miwili na kuna mpango wa kuanzisha  mtaa wa viwanda mwingine kwa kuhuisha eneo lilokuwa kiwanda cha General tyre ambao utakuwa moja ya mtaa mkubwa wa viwanda nchini.

 

Prof. Mkumbo wakati akitoa taarifa ya kanzi data ya viwanda nchini ameeleza kuwa  hadi kufika mwezi Julai 2021 Tanzania ina jumla ya viwanda 80,969 nchini nzima ikiwemo viwanda 2,935 vilivyopo Arusha na kati hivyo viwanda 618 ni vikubwa.