Habari
MRADI MKUBWA WA LNG LINDI WAINGIA HATUA ZA MWISHO ZA MAJADILIANO YA KIMKATABA
Serikali ipo mbioni kukamilisha majadiliano ya kimkataba kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (TLNG), unaotekelezwa kwa ushirikiano na Kampuni za Kimataifa za Nishati (IECs).
Hayo yameelezwa Januari 30, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lindi Mjini, Mhe. Mohamed Utaly, kwa niaba ya Waziri wa Nishati.
Katika swali lake, Mbunge Utaly alihoji ni lini ujenzi wa mradi wa LNG utaanza pamoja na hatua zilizofikiwa hadi sasa ili kuhakikisha mradi huo unaanza kama ilivyopangwa.
Akijibu, Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi huo na kwa sasa umefikia hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya mikataba mbalimbali ya utekelezaji.
Ameeleza kuwa mara tu majadiliano hayo yatakapokamilika, utekelezaji wa mradi utaanza rasmi, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha sekta ya nishati nchini.
