Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mhe. Kigahe awahimiza Watanzania kutumia fursa ya kuuza na kununua bidhaa mbalimbali kupitia mtandaoni.


Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema kuwa ni muda muafaka kwa  Watanzania kutumia fursa ya kuuza na kununua bidhaa mbalimbali kupitia mtandaoni.

Hayo ameyasema Machi 9, 2023 alipomwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) katika hafla ya ufunguzi wa kampuni ya mtandaoni ya DU-BUY.COM kutoka nchi ya falme za kiarabu Dubai.

Mhe. Kigahe ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha watanzania wanatumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa hasa soko la eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA), soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na soko la SADC.

“Kampuni hii kutoka nchi ya falme za kiarabu ya Dubai inayomilikiwa na kampuni mama ya DP World wanakuja kufungua ofisi zao nchini Tanzania ambapo itatuongezea ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Dubai na nchi nyinginezo hivyo watanzania tutumie fursa ya kufanya biashara mtandaoni katika kununua na kuuza bidhaa mbalimbali” Amesema Mhe. Kigahe.

Nao wamiliki wa kampuni ya DU-BUY kutoka Dubai wameishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano waliopewa hasa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji wa biashara ya mtandaoni ambapo watanzania wataweza kuagiza na kuuza bidhaa zao kupitia mtandao katika nchi zaidi ya 78 Duniani.