Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mhe. Kigahe (Mb) amuhakikishia mwekezaji wa kiwanda cha TROLLE MEES LE TANZANIA IVS LTD soko la uhakika la mafuta ya mawese.


Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb)  amemuhakikishia mwekezaji wa kiwanda cha  TROLLE MEES LE TANZANIA IVS LTD soko la uhakika la mafuta ya mawese baada ya kuanza utekezaji wa kutatua  changamoto  zilizojitokeza kwenye ziara ya Mhe Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 
 
Mhe Kigahe ameyasema hayo Machi 26, 2023 Mkoani Kigoma wakati wa kupokea taarifa ya kamati ya kufanya tathimini ya changamoto zilizojitokeza katika kuongeza thamani ya zao la mchikichi mkoani Kigoma. 
 
Akiwa mkoani Kigoma tarehe 27 Februari ,2023 Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) alipokea changamoto anuai kutoka kwa mwekezaji anaejenga kiwanda cha kuchakata na kuongeza thamani mafuta ya mawese cha TROLLE MEES LE TANZANIA  IVS LTD kinachomilikiwa na Bw. Abdalah Mwilima.
 
Aidha changamoto zilizoainishwa na mwekezaji huyo ni pamoja na  upungufu  malighafi ya zao la mchikichi,  Eneo la kupanda zao la mchikichi  na umeme kutokuwa na nguvu ya kutosha kuendesha mitambo iliyofungwa  kiwandani hapo,  Kutopata kiasi chote cha mkopo alichoomba katika benki  ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).
 
Kutokana na changamoto hizo, Mhe Waziri Mkuu aliagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake ikiwemo SIDO kushughulikia changamoto zote zilizoanishwa na kuzipatia ufumbuzi  kwa wakati.
 
Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya kamati hiyo Mhe. Kigahe amemuhakikishia mwekezaji huyo kuwa Wizara imepokea changamoto zote zilizoanishwa na  kuzifanyia kazi kwa haraka huku  baadhi zikiwa zimepatiwa ufumbuzi tayari na zingine zikiwa bado  kufanyiwa kazi.
 
“Naomba nikuhakikishie kuwa changamoto zote  tumeanza kuzifanyia kazi baada ya kupokea maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB) imeshafanyia kazi changamoto ya  kifedha  imeshatatuliwa, kuhusu changamoto ya umeme tumeongea na Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kigoma  anafanyia kazi  kwa uharaka zaidi" Alisema Mhe. Kigahe
 
Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara  Dkt. Hashil Abdallah amemhakikishia Naibu Waziri utekezaji wa changamoto  zilizoanishwa kwa kusema kuwa, atahakikisha zao la mchikichi linawakwamua Wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwa ndilo zao la kimkakati katika mkoa huo.
 
“Tunataka viwanda vyetu vitumie mafuta ghafi kutoka katika viwanda vyetu kikiwemo kiwanda hiki cha TROLLE MEES LE TANZANIA  IVS LTD Tunataka wakulima wanaozalisha mchikichi kutoka mkoa wa Kigoma wawe na uhakika wa kuzalisha zaidi, sababu soko litakuwepo la uhakika  lakini hata mzalishaji atakuwa na uhakika wa kuzalisha zaidi maana atakuwa na uhakika wa malighafi” Alisema Dkt Abdallah.