Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mhe. Kihage atoa wito kwa watoa huduma ya nishati jadidifu wanaouza vifaa kwa kukupesha kwa wananchi.


Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), amewataka  watoa huduma ya nishati jadidifu wanaouza vifaa kwa kuwakopesha wananchi kwa njia ya mikataba, kuwasiliana na Tume ya Ushindani (FCC) kupitia kwa Maafisa Biashara wa Mikoa, Wilaya, Manispaa na Majiji ili kuhakikisha Mikataba yao inawasilishwa FCC kwa mapitio na usajili kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha Sheria ya Ushindani (Na. 8 ya mwaka 2003), ikisomwa kwa pamoja na kanuni za kudhiti mikataba ya watumiaji inayoandaliwa na upande mmoja za mwaka 2014.

Mhe. Kigahe aliyasema hayo alipomwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), katika kilele cha maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya haki za Mtumiaji Duniani yaliyofanyika jijini Mbeya Machi 15, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya royal tughimbe.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika chini ya Kaulimbiu “Nishati Safi kwa Ustawi wa Mlaji na Mazingira” pia alitoa rai kwa FCC kushirikiana kwa karibu na sekta za uzalishaji wa nishati kwa kuhakikisha wazalishaji hao wanazalisha nishati safi zinazozingatia haki za mlaji na zisizoharibu mazingira na kuimarisha ustawi wa bioanuwai na ekolojia.

Aidha, aliitaka FCC kushirikiana na Baraza la Usimamizi na Utunzaji Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) katika kutekeleza jukumu hilo.

Akizungumzia mafanikio ya kihistoria katika eneo la nishati ya umeme nchini, Mhe. Kigahe alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu shupavu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kukamilisha miradi mbalimbali ya nishati nchini ikiwa ni pamoja na mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Nyerere ambao unalenga kuzalisha umeme wa Megawati 2,115 kwa gharama ya Dola za Marekani Bilioni 2.77, sawa na Shilingi za Tanzania Trilioni 6.55/- hadi utakapokamilika mwaka 2024. 

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC), Dkt. Aggrey Kalimwage Mlimuka alisema kuwa siku ya Haki za Mtumiaji Duniani huadhimishwa ifikapo Machi 15 kila mwaka ili kuwakumbusha walaji, wazalishaji wa bidhaa na watoa huduma umuhimu wa kuzingatia haki za watumiaji katika soko.

Alisema vikao vya viongozi wa dunia ikiwemo Mkutano wa Mazingira uliofanyika katika Mji wa Sharm El Sheikh nchini Misri, Novemba, 2022, uliohudhuriwa na Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, vilisisitiza umuhimu wa kuihami dunia dhidi ya uharibifu wa mazingira na kusisitiza umuhimu wa kushajiisha matumizi ya nishati safi duniani.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Zaytun Kikula, amesema kuwa jamii yetu imekuwa ikitumia nishati kwa ustawi wao ambapo wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo nishati hiyo kupatikana kwa gharama kubwa, jambo linalochochea uharibifu wa mazingira kwa kuwafanya wahamie katika nishati zinazotokana na kuni na mkaa.

Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Halali wa Kibiashara, Zanzibar (ZFCC) Bw. Mohammed Sijamini Mohammed, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani Tanzania Bara, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, Mkurugenzi Mkuu wa Kwanza wa FCC Bw. Godfrey Enock Mkocha (aliyekuwa mmoja wa watoa mada), Makamishina wa FCC, Maafisa Tawala Wasaidizi wa Biashara na Shughuli za Kiuchumi kutoka Ofisi za Mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali, wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jijini Mbeya (MUST).

Sambamba na ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Kigahe alikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa ofisi ya FCC kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hatua ambayo ni mwendelezo wa juhudi za FCC za kupeleka huduma zake karibu zaidi na wananchi.