Habari
WAZIRI KAPINGA AKUTANA NA HUAWEI, WAJADILI NAMNA YA KUKUZA BIASHARA KUPITIA TEHAMA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Biashara wa Huawei, Bw. Vicent Wen, tarehe 17 Machi 2026 jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na kampuni hiyo katika kutekeleza programu mbalimbali za kibiashara kupitia TEHAMA, sekta ambayo kwa sasa ina mchango mkubwa katika kuzalisha ajira na kukuza maendeleo ya viwanda na biashara nchini.
Aidha, waligusia umuhimu wa ushirikiano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kuendeleza ujuzi wa TEHAMA, kukuza ubunifu wa kidijitali pamoja na uundaji wa maudhui (content creation) na kutambua vipaji vya vijana.
Pia, walijadili haja ya kuhakikisha uendelevu wa programu za Huawei hapa nchini, hususan zile zinazoendelea kutekelezwa kama DigiTruck na Talent ICT Program, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uwezo wa wananchi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
