Habari
KAPINGA AIAGIZA TBS KUONGEZA KASI NA UBUNIFU KATIKA KULINDA UBORA NA USALAMA WA BIDHAA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), ametoa wito kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake kwa ubunifu na ushirikiano.
Ameyasema hayo Novemba 27, 2025 alipotembelea Shirika hilo, akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Dkt Suleiman Serera pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw. Sempeho Manongi, na kuzungumza na Bodi na Menejimenti ya TBS ambapo aliwaahidi ushirikiano katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama.
Aidha, Waziri Kapinga ameisisitiza TBS kutoa huduma zenye matokeo kwa Watanzania, kwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kulinda afya na kipato cha Watanzania.
Waziri kapinga pia ameiagiza TBS kuendeleza Programu za uelimishaji wa Viwango kwa wananchi na kuhakikisha mifumo inasomana ndani ya ya Shirika hilo na Taasisi za nje ili kudhibiti ubora wa bidhaa kwa kushirikiana na FCC.
Aidha, amesisitiza TBS kukamilisha miradi kwa wakati ili kuboresha utoaji huduma kwa ufanisi, huku akitaka wakandarasi wasimamiwe ipasavyo na miradi isogeze huduma kwa wananchi bila kuongeza gharama au kupoteza muda.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera amesisitiza Menejimenti hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na weledi ili kutekeleza majukumu yake Shirika hilo kwa ufanisi.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS Bw. Hussein Sufian ameahidi kuwa Bodi hiyo iko tayari kupokea na kutekeleza Maelekezo hayo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi amebainisha kuwa Shirika limekuwa linashirikiana na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara zingine nchini ili kuhakikisha linatekeleza shughuli zake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa Watanzania.
