Habari
WAZIRI KAPINGA: USHIRIKIANO WA TANZANIA NA EU UFUNGUE MILANGO YA KIUCHUMI NA SIO UTEGEMEZI
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), wanakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa.
Waziri Kapinga aliyasema hayo Mei 7, 2026, wakati wa maadhimisho ya Europe Day yaliyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu “Gateway to Growth”, ambapo viongozi mbalimbali, mabalozi, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa walishiriki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kapinga alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya umeendelea kukua kwa zaidi ya miaka 50 kutoka ushirikiano wa maendeleo hadi kuwa ushirikiano mpana unaojumuisha biashara, uwekezaji, miundombinu na ukuaji wa sekta binafsi.
Ameeleza kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuweka mazingira bora ya biashara, kuongeza ushindani wa viwanda na kuvutia wawekezaji.
“Tunataka kuondoka zaidi kwenye utegemezi wa misaada na kuelekea kwenye biashara, uwekezaji na ujenzi wa mifumo ya uzalishaji yenye kuongeza thamani ndani ya uchumi wetu”.
Alisema Tanzania inanufaika na ushirikiano huo kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa kijani, miundombinu, mifumo ya kidijitali, uchumi wa buluu, nishati pamoja na maendeleo ya biashara na viwanda.
Aidha, Waziri huyo alisema Tanzania ipo katika nafasi nzuri kimkakati kutokana na eneo lake, masoko ya kikanda, ongezeko la watu, rasilimali zilizopo na ukuaji wa sekta ya viwanda, hali inayofanya nchi kuwa lango muhimu la biashara kwa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.
Katika hotuba yake, Waziri Kapinga aliwatambua wafanyabiashara wadogo na wa kati kuwa msingi muhimu wa uchumi kwa kuwa wanatoa ajira, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kufungua fursa kwa vijana na wanawake.
Alisema serikali itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuhakikisha biashara hizo zinapata mitaji, masoko, teknolojia na mazingira rafiki yatakayowasaidia kukua na kushindana kimataifa.
