Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Bidhaa zote nchini zinasajiliwa kwa kutumia barcode ili kuziwezesha kupata soko la ndani na nje ya nchi.


Waziri wa Viwanda na Biashara Mh.Dkt.Suleiman Jafo(Mb) ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) @tbs_viwango na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) @brela_tanzania kuhakikisha bidhaa zote nchini zinasajiliwa kwa kutumia barcode ili kuziwezesha kupata soko la ndani na nje ya nchi.

Amebainisha hayo wakati wa utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya taasisi za Serikali zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara TBS, BRELA pamoja na GS1 Tanzania Mei 20,2025 jijini Dar es Salaam.

Aidha Dkt.Jafo amesema kuna umuhimu wa usajili wa barcode kwa bidhaa zote zinazozalishwa hapa nchini kwani kutaiwezesha serikali na wizara kufuatilia mapato ya uzalishaji wa taifa na kukusanya takwimu za uhakika za bidhaa zote zinazozalishwa Tanzania na kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi za kupanga na kukuza uchumi.

Dkt. Jafo pia ameeleza kuwa ushirikiano huo utaleta ushirikiano bora kati ya taasisi, hatimaye kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania na kuongeza ushindani wa kimataifa wa bidhaa zinazotengenezwa na Tanzania.

Vilevile ameongeza kuwa Serikali ina matumaini kwamba mpango huo mpya wa barcode utawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kupata soko la bidhaa zao kimataifa zaidi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa GS1 Tanzania Bi. Fatuma Kange amesema ushirikiano huo utaimarisha mchakato wa usajili wa biashara ndogo na za kati (SMEs) kabla ya kubadilika na kuwa viwanda vikubwa na utaziwezesha taasisi kama BRELA na TBS kukusanya takwimu muhimu za wateja, zikiwemo kutoka kwa wafanyabiashara ambao bado hawajatekeleza misimbo hiyo na kuongeza mwonekano wa biashara kupitia chapa, na kwa wale waliosajiliwa na BRELA, watapata fursa ya kupata chapa ya bidhaa, alama za biashara na vyeti ambavyo ni muhimu kwa kutambulika sokoni,

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesisitiza kuwa Makubaliano hayo yataleta manufaa makubwa katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuongeza elimu ya biashara kwa wajasiriamali, kuendeleza tafiti za haki miliki na kupanua wigo wa soko la bidhaa zinazozalishwa nchini.