Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Waziri wa Viwanda na Biashara Sisitiza Umuhimu wa Haki Miliki za wataaluma


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt. Selemani Jafo ( Mb) ameagiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa miliki bunifu na kusisitiza usajili wa bunifu hizo ili kuwalinda wabunifu na wasanii nchini.

Amebainisha hayo kwwnye maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani yenye Kauli mbiu isemayo“Miliki Bunifu na Muziki: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu”, Mei 21,2025 jijini Dar es Salaam,

Waziri Jafo alisema wasanii wa muziki na wabunifu wa aina mbalimbali wanapaswa kutambua kuwa usajili wa bunifu ni hatua muhimu ya kuhakikisha wanafaidika na kazi zao wakiwa hai, na hata baada ya kufariki, warithi wao watanufaika.

Waziri Jafo ameeleza kuwa sekta hiyo ni kichocheo cha ajira kwa vijana, kwani serikali haiwezi kuajiri watu wote. Kwa mujibu wake, serikali inaweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi ziweze kustawi.

Katika hatua nyingine, ameeleza mpango wa ujenzi wa viwanda 9,048 katika kila mkoa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwishoni mwa mwaka huu hadi mwaka 2031. Mpango huo unalenga kutoa ajira kwa vijana milioni 6.5.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya BRELA, Prof. Neema Mori, ameeleza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia na kuweka mikakati ya kutoa elimu kwa wabunifu ili kuwajengea uelewa wa namna ya kusajili na kunufaika na kazi zao.

Prof. Mori ameongeza kuwa BRELA inashirikiana na taasisi mbalimbali kama COSOTA, BPRA na COSOZA kuweka mazingira bora ya kulinda na kuhamasisha matumizi sahihi ya miliki bunifu.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alitoa rai kwa wasanii na wabunifu kusajili majina ya bidhaa na huduma wanazotoa kupitia brand zao ili kuyalinda kisheria