Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

ZIARA YA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA NCHINI CHINA YAZAA MATUNDA


Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China zimefikia hatua muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi, kufuatia makubaliano ya kuanzishwa kwa kiwanda cha kisasa cha kuchakata Kemikali nchini Tanzania, kitakachogharimu takribani Dola za Marekani milioni 500.

Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara ya kikazi ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), nchini China, ambapo juhudi zake zimeanza kuzaa matokeo chanya katika kuvutia uwekezaji wa kimkakati.

Machi 23, 2026, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara hiyo, Waziri Kapinga ametembelea Guangdong na kufanya ziara katika kampuni kubwa ya kuchakata Kemikali.

Akiwa nchini China, amepata fursa ya kukutana na uongozi wa kampuni hiyo na kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, hususan katika sekta ya viwanda na uhifadhi wa mazingira.

Kufuatia majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo akatangaza nia ya kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kisasa cha Kemikali.

Ameeleza kuwa kiwanda hicho kitakuwa cha kwanza barani Afrika, hatua itakayoweka Tanzania katika nafasi ya kipekee ya kiteknolojia na kimazingira.

Mradi huo mkubwa unatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kulinda mazingira, pamoja na kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi.

Ziara hii inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kukuza uchumi kupitia uwekezaji wa viwanda endelevu.