Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Mkesha wa kuliombea Taifa uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam.


MHE. INNOCENT BASHUNGWA AONGOZA MAMIA YA WATANZANIA KATIKA MKESHA WA KULIOMBEA TAIFA LA TANZANIA KATIKA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2020. Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa ameongoza mamia ya watanzania katika mkesha wa kuliombea Taifa la Tanzania uliofanyika usiku wa Jumanne tarehe 31 Desemba, 2019 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Katika mkesha huo wa kuukaribisha mwaka mpya 2020 uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa dini ambapo waliongoza kwa dua na maombi kuliombea taifa letu, hasa viongozi waliobeba dhamana ya kuwatumikia watanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Akihutubia umati huo, Mhe. Bashungwa ambaye alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, alisema kwamba lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kunufaisha Watanzania. Katika kufanikisha hilo, Serikali inaendelea kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, maji, umeme, huduma za afya, elimu n.k Aidha Mhe. Bashungwa alisema kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha rasilimali za kilimo na utalii zinanufaisha wananchi walio wengi na sio wachache. Akitolea mfano kwenye sekta ya viwanda na biashara, maboresho yamefanyika BRELA, TBS na EPZA na kubainisha kuwa tayari fidia imekwishalipwa kwa ajili ya kujenga eneo maalumu la uchumi Kurasini litakalotumika kuchakata mazao ya kilimo na kutengeza ajira kwa kina mama na vijana ili kukuza uchumi wa nchi. Katika mkesha huo Askofu Mkuu wa Tanzania Fellowship of Church (TFC) ndugu Godfrey Malasi alisema kuwa viongozi walioteuliwa na Mhe. Rais Magufuli, wana jukumu la kumsaidia huku wakiendana na kasi ya awamu ya tano na sio kumbebesha mzigo kwa kutotimiza wajibu wao kiutendaji. Malasi alisema kuwa uelewa mdogo wa wananchi katika kusaidia kusukuma kasi ya uchumi wa viwanda imekuwa ni changamoto katika kuongeza kasi ya maendeleo kwani wamegeuka kuwa wachuuzi badala ya wazalishaji wa bidhaa hizo. Alisema kuwa kauli mbiu ya Tanzania ya viwanda inamtaka kila mmoja kushiriki kikamilifu na siyo kuzurura mtaani ukiuza vifaa vya urembo badala ya kwenda kulima na kuzalisha mazao. “Neno la Mungu linasema asiyefanya kazi na asile, ukimuona mtu ananing’iniza ushaga mwambie aende vijiji akalime tupate mazao sababu mambo ya kuning’iniza shanga haliwezi kuleta mabadiliko yoyote kwenye Tanzania ya viwanda,” alisema Mkesha huo wa Kitaifa uliandaliwa na kuratibiwa na mashirika ya dini (Tanzania Fellowship of Churches) kwa Kushirikiana na Makanisa na huduma mbalimbali. MWISHO Imetolewa na: Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Wizara ya Viwanda na Biashara, 31 Desemba, 2019