Habari
Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb.) akiwa na Mawaziri wenzake ameshiriki Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayojumuisha Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Somalia unaofanyika Makao Makuu ya Afrika Mashariki Novemba 28, 2024 jijini Arusha.
Waziri Jafo ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Julai 2024, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Deng Alor Kuol amewapongeza Mawaziri kwa kushiriki mkutano huo na kuwaomba kutoa michango yao chanya katika agenda zilizowasilishwa kwao kabla ya kuziwasilisha kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC utakaofanyika tarehe 29 na 30 Novemba 2024.
Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa EAC, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira; taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2024 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha, pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2025.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na umejumuisha Mawaziri wengine Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara husika