Habari
Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi yanalenga kukuza uchumi wa nchi

Katika kuhakikisha lengo la kukua kwa uchumi na kufikia lengo la asilimia 8 nchini Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na Wadau katika Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wameandaa Mkutano wa majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi utakaofanyika kesho Februari 2, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Julius Nyerere International Conference Centre – JNICC) Jijini Dar es Salaam huku Mgeni Rasmi na Mzungumzaji Mkuu akitarajiwa kuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji (Mb.)
Akizungumza na waandishi wa habari leo tar 01 Januari, 2023 jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema mkutano huo unalenga kufanya majadiliano ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
” Tumekuwa tukifanya mikutano na mijadala mbalimbali ambayo inaakisi dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kukuza na kuimarisha majadiliano na ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.” Amesema.
Pia amesema, Ili kuendelea kukuza biashara na uwekezaji nchini, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Mazingira ya Biashara nchini (MKUMBI) na kuboresha upatikanaji wa miundombinu na huduma wezeshi kama vile gesi asilia, ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, umeme, maji na ardhi kwa wawekezaji.
Aidha ameeleza kuwa, mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa mwaka 2023 umebeba Kauli mbiu ya “Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Uchumi wa Tanzania”.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara Dkt. Godwill Wanga amesema, suala la uboreshaji wa Biashara na mazingira ya Uwekezaji ni muhimu hasa katika ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Vilevile Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF Octavian Mshilu amesema Serikali inafanya kazi kubwa hususan ya kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara na TPSF inaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Serikali ili kukuza uchumi wa watanzania na Nchi kwa ujumla.
Aidha amewataka watanzania, wafanyabiashara na wawekezaji waliopo ndani na nje ya nchi kufuatilia mkutano huo na kushirikisha fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Mkutano huo utawakutanisha na washiriki zaidi ya 500 ukijumuisha Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Viongozi Wakuu kutoka Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mawaziri wa Kisekta, Makatibu Wakuu wa Wizara za kisekta, Wenyeviti wa Kongani mbalimbali, wamiliki wa kampuni, wamiliki wa viwanda, Vyama vya Sekta Binafsi, Jumuiya za Wafanyabiashara, wawekezaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati, Wakuu wa Taasisi za Serikali, watafiti wabobezi, watunga sera, washirika wa maendeleo na Asasi za Kiraia (AZAKI).