Habari
Naibu Waziri Wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema Serikali ilibaini kuwa Wadai hawana haki ya kulipwa na Serikali marupurupu yanayotokana na Mkataba wa Hiari

Naibu Waziri Wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema Serikali ilibaini kuwa Wadai hawana haki ya kulipwa na Serikali marupurupu yanayotokana na Mkataba wa Hiari kwa sababu madai hayo hayapo kwenye orodha ya malipo yanayostahili kulipwa na Serikali chini ya sheria inayoongoza urekebishaji wa mashirika ya umma.
Kigahe amesema hayo Juni 26,2023 Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Ester Edwin Maleko kuhusu ni lini Serikali itawalipa mafao ya Watumishi waliokuwa Kiwanda cha Magunia Moshi.
Amesema kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ilipokea madai ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Magunia Moshi na kuyashughulikia kwa kuunda Kamati ya Uhakiki ambayo ilibainisha kuwa Watumishi hao walishalipwa mafao yao na kujulishwa kwa barua yenye Kumb. Na. CKB.87/406/02/C/80 ya tarehe 3 Mei 2019.
Aidha Kigahe amesema kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo zinaonesha kuwa waliokuwa wafanyakazi hao walilipwa stahili zifuatazo: mshahara wa mwezi mmoja,malimbikizo ya likizo, malimbikizo ya mishahara, gharama za kusafirisha mizigo, na malimbikizo ya michango ya akiba kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii.