Habari
Naibu waziri wa viwanda na biashara azindua kiwanda cha kuchakata zabibu cha WENDECE,

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mhandisi STELLA MANYANYA (Mb), amesema kunahaja ya kuziwezesha kifedha taasisi za utafiti zinazobuni na kutekeleza teknolojia rahisi hapa nchini ili kufikia lengo la kuwa na viwanda na kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Naibu Waziri Manyanya ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua teknolojia mpya ya mashine ya kukamua mchuzi wa zao la zabibu katika kiwanda kidogo Cha WENDECHE kilichopo Kata ya Hombolo Bwawani, iliyobuniwa na TEMDO kwa kushirikiana na SIDO. Alisema Kuna haja ya kuziwezesha taasisi Kama SIDO, TEMDO, CAMATEC, TIRDO na nyiinginezo, kwani kwa muda mrefu taasisi hizo zilikuwepo lakini hazikuweza kutunufaisha, lakini tangu zimewezeshwa kifedha tayari matokeo yameanza kuonekana. "Hii inafurahisha sana hizi taasisi zimewezsshwa na matokeo chanya tumeyaona, "Alisema Manyanya. Alisema hivi sasa taasisi hizo zinatia moyo kutokana na kwamba zimewezeshwa na zimeweza hivyo zinapaswa kuangaliwa kwa karibu sababu zitasaidia zaidi ukuaji wa viwanda nchini. Aidha amewahimiza watanzania kuthamini vitu vinavyotengenezwa hapa nchini, ikiwamo kuthamini viwanda vidogo kwa sababu vinasaidia kutoa ajira kwa watanzania, huku akiitaka SIDO kuhakikisha inasimamia wenye viwanda vidogo kuhakikisha wanapata mikopo kutoka benki ya kilimo Tanzania, TIDB, ili kuviongezea nguvu. Alisema hakuna haja ya kubaki nyuma tunafanya kile tunachoweza na baadae kitaleta matokeo makubwa hapo baadae na kufikia Tanzania ya viwanda kama ilivyokusudiwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John P. Magufuli. Alisema ni vema SIDO wakaweka jitihada ya kuwa karibu na watu hao ambao wakiwezeshwa wanaweza kuleta matokeo chanya katika kile ambacho wanafanya. Mbali na hilo Naibu Waziri Manyanya amewapa Wiki tatu TEMDO kuhakikisha wanawatengenezea mashine wajasiriamali ambao walitoa oda ya kutengenezewa mashine ili nao waendelee na shughuli ya uchakataji wa zabibu kwani mashine hizo ni nzuri na zina ufanisi wa hali ya juu. Alisema hakuna sababu ya kuwacheleweshea kwa sababu wanahitaji kwa ajili ya kufanya maendeleo. Kwa upande wake Meneja Taasisi ya ubunifu na uhandisi Mitambo, TEMDO, Mhandisi Alexander Komba, alisema kazi yao ni kubuni na kuendeleza Technolojia kwa ajili ya wajasiliamali wazalishaji, Kisha kupeleka kwa SIDO ili ziweze kuwafikia walengwa, na waliweza kutatua changamoto ya kuchakata zao la Zabibu kwa haraka. Alisema lengo lao ni kuona watu hao wanasonga mbele na si kurudi nyuma.