Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MKAKATI MPYA: VIONGOZI WA DINI KUSHIRIKISHWA KUTOA ELIMU YA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeihimiza Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuwashirikisha Viongozi mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Dini katika kutoa elimu ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuondoa upotoshaji na kuongeza uelewa kwa Wananchi kuhusu Mfumo huo.

Hayo yamesemwa Aprili 27, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kenneth Nollo (Mb), wakati wa mafunzo ya uelewa kuhusu kazi za Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kwa Kamati hiyo ambapo amepongeza kuwa upanuzi wa Mfumo huo kuelekea sekta ya mifugo utasaidia kukomesha unyonyaji wa walanguzi ambao wamekuwa wakiwadhulumu wafugaji kwa muda mrefu.

Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mhe. Emmanuel Cherehani, wamepongeza jitihada za Serikali na kushauri nguvu kubwa ielekezwe vijijini ambako ndiko chimbuko la uzalishaji. Wameeleza kuwa kuingizwa kwa mifugo katika Stakabadhi za Ghala kutawawezesha wafugaji kutumia wanyama wao kama dhamana ya kupata mikopo na kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mifugo hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amebainisha kuwa Serikali inapambana na changamoto za kisaikolojia miongoni mwa wakulima ambao bado wana hofu ya kutumia Mfumo huo kutokana na migogoro ya zamani ya Ushirika.

 Amewaomba Wabunge kuwa mabalozi katika majimbo yao ili kuwahamasisha Wananchi kuchangamkia fursa za Mfumo huo ambao ni salama na wenye tija kwa uchumi wa Kaya na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amefafanua kuwa kuanzishwa kwa risiti za kielektroniki kumesaidia kuongeza uwazi na kuifanya Tanzania kupata heshima ya kimataifa, ikiwemo nchi ya Nigeria kutaka kuja kujifunza Mfumo huo. Ameeleza kuwa hadi sasa zaidi ya tani milioni tano za bidhaa zimeuzwa kupitia mfumo huo, huku zao la korosho likiongoza kwa kutoa mchango mkubwa katika mauzo ya nje.

Hata hivyo, Bw. Bangu amebainisha kuwa bado kuna vikwazo kama vile miundombinu mibovu ya maghala na uaminifu mdogo wa baadhi ya watendaji, mambo ambayo mamlaka inayashughulikia kwa karibu. Amewahakikishia wadau kuwa WRRB inaendelea na mazungumzo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha sekta zote muhimu zinaingizwa kwenye mfumo huo kwa manufaa ya Taifa zima.