Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAFANYABIASHARA WA OMAN WAVUTIWA NA MAGARI YANAYOTENGENEZWA TANZANIA


Balozi wa Tanzania anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati, Mhe. Bw. Abdallah Kilima alisema Ujumbe wa Wafanyabiashara wa Oman waliotembelea nchini wamevutiwa na ubora wa magari yanayozalishwa na Kiwanda cha Kuunganisha Magari cha Sartun pamoja na teknolojia inayotumika.

Balozi Kilima ameyasema hayo Septemba 09, 2025 wakati wa ziara ya Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka Oman waliotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea shughuli za Uzalishaji kiwandani hapo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda Bw. Juma Mwambapa, kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, alisema Serikali imekuwa na nia thabiti ya kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na tayari imeshuhudia mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Oman Bw. Yagoob Al Rabaani alifurahishwa kuona kuwa Tanzania ina uwezo wa kuunganisha magari yenye ubora wa hali ya juu katika kiwanda kizuri hicho kilicho na viwango vya juu.

“Tunataka ushirikiano, Nchini Oman tuna maeneo ya free zone, hivyo tunaweza kushirikiana na pia kuhamishia teknolojia hii Oman ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu,” alisema Bw. Al Rabaani

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sartun, Bw. Rehmatullah Habib, alisema imejenga karakana mpya kwa ajili ya kutengeneza baadhi ya vipuri vya magari, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kukuza viwanda vya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Bw. Habib alieleza kuwa tangu uzinduzi wa kiwanda hicho mwaka jana, mauzo ya magari yameongezeka kutoka magari 200 hadi 1,800 kwa sasa na wanatarajia kukuza Magari magari 3,000 kwa mwaka

Tunashukuru Serikali kwa kuongeza ushuru wa Industrial Development Levy kwa magari yanayoagizwa kutoka nje, hatua iliyosaidia kuinua viwanda vya ndani,” aliongeza.