Habari
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA UTEKELEZAJI WA BAJETI 2025/2026
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, kilimo na mifugo imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwenendo mzuri wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali vya wizara hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), Machi 24, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti 2025/2026 kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kubainisha kuwa ushirikiano unaotolewa na Wajumbe ndani ya Kamati hiyo ndio nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya Wizara hiyo.
Nao Wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utekelezaji wa Miradi hiyo kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (MB), amesema Wizara yake inaendelea na utekelezaji wa mipango mbalimbali ikiwemo ufufuaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini, Udhibiti wa ufungashaji wa mazao, kulinda biashara za wazawa pamoja na utekelezaji wa mradi wa uchimbaji chuma wa Liganga na Mchuchuma na ule wa Magadi soda wa Engaruka ambapo mpaka sasa tayari wananchi wameshalipwa fidia ili miradi hiyo iweze kuanza utekelezaji
