Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

PIC Yaipongeza TIRDO


PIC Yaipongeza TIRDO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefurahishwa na utendaji wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) na kuiagiza iendelee kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia ubunifu wa teknolojia hasa katika uzalishaji wa bidhaa nchini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jerry Silaa 20 Oktoba, 2022 wakati wa kupokea na kujadili taarifa ya Utekelezaji wa majukumu ya Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) Bungeni jijini Dodoma.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara; Dkt. Hashil Abdallah alilihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara itaendelea na jukumu la kuisimamia Taasisi ya TIRDO katika kuhakikisha inafikia malengo yake hasa katika kubuni teknolojia na kufanya tafiti mbalimbali kwa maendeleo ya Viwanda.

 Mwenyekiti wa Baraza la Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO); Mhandisi Bashir Juma Mrindoko ameiahidi Kamati hiyo kuwa Shirika litafanyia kazi maoni na maelekezo yote yaliyotolewa ili kulifanya Shirika hilo kuwa kitovu cha teknolojia kwa maendeleo ya Viwanda nchini.

Awali akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Shirika, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO; Prof. Mkumbukwa M. Mtambo amesema kuwa Taasisi yake ina watumishi 88 walio katika kada mbalimbali wakiwemo wahandisi, watafiti, mafundi mchundo na wataalamu mbalimbali.

Prof. Mtambo amesema kuwa TIRDO imejikita katika kutafiti na kubuni tekinolojia mbalimbali za uendelezaji viwanda ikiwemo ya kuchakata taka za plastiki ambayo kuongeza ajira kwa watanzania 

Prof. Mtambo amesema kuwa Shirika la TIRDO limesaidia Serikali katika tafiti mbalimbali ikiwemo ya upimaji wa makaa ya mawe, tafiti ambayo ilionesha makaa ya mawe ya Tanzania ni bora zaidi hivyo kupelekea kusitishwa uagizaji wa makaa hayo nje ya nchi.

Aidha Prof Mtambo emeeleza  kuwa, Usitishwaji huu ulipelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa makaa ya mawe kutoka katika migodi yetu iliyopo Ngaka katika Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyetu nchini na uuzaji nje ya Nchi.

“Shirika la TIRDO limehusika katika kufanya tafiti ya madini ya chuma cha Liganga Ludewa Mkoani Njombe ambapo walibaini kiasi halisi cha madini ya chuma ambacho ni zaidi ya asilimia 70 na kufanikiwa kugundua madini mengine yanayopatikana kama Vanadium, Titanium na Aluminium ambayo hayakutajwa katika mkataba wa awali wa tafiti iliyofanyika”. Amesema Prof. Mtambo.