Habari
Sekta Binafsi tumieni fursa za Afrexim Bank Kanda ya Afrika
Sekta Binafsi tumieni fursa za Afrexim Bank Kanda ya Afrika
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Suleiman Serera ameishauri sekta binafsi ya Tanzania kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa Benki ya Kanda ya Afrika ya Afrexim kupata mitaji itakayowezesha kuongeza thamani mazao na bidhaa za viwandani kwa kiwango cha kimataifa na kukidhi ushindani katika soko la Afrika
Dkt. Serera ameyasema hayo Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Waandishi wa Habari baada ya kufungua Kowngamano la Afreximbank Roadshow lililoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Benki hiyo likilenga kutambua changamoto za wafanyabiashara na kuzitatua kupitia fursa za mitaji, fursa za masoko na teknolojia
Aidha, Dkt. Serera alihimiza Sekra hiyo binafsi kushirikiana na Afreximbank na kutumia fedha zinazopatikana kwa usindikaji wa mazao ya kilimo, maendeleo ya mauzo ya nje, ujenzi wa viwanda vya kijani, na biashara ya kikanda.
"Tuwekeze Dodoma, Mbeya, na Kigoma," alihimiza. "Tujenge Maeneo ya Usindikaji wa Mauzo ya Nje, tuimarishe korido za vifaa, na tujenge miundombinu ya kidijitali kwa mfumo wa biashara unaostawi."
Kwa upande wake Rais wa TCCIA Bw. Vincent Minja amesema kongamano hilo ni muhimu katika uwezeshaji wa biashara barani Afrika kwa kuwa biashara kati ya nchi za Afrika bado ni kidogo ikilinganishwa na biashara kati Afrika na na mabara mengine duniani
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Uhusiano wa Wateja wa benki hiyo Bw. Eric Monchu ameihakikishia sekta binafsi ya Tanzania kuwa wako tayari kukuza uchumi endelevu wa Tanzania na hadi sasa, Benki hiyo imetoa takriban dola bilioni 2 kuwezesha utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati nchini ikiwemo Dola milioni 800 kwa kwa ajili ya Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, Dola milioni 290 kwa Reli ya SGR na Dola milioni 200 kwa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade) Bi Lulu Mkude amewaalika wadau na mabenki mbalimbali waliohudhuria kongamano hilo kushiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam yatakayoanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2025 kwani ni jukwaa zuri la kutangaza biashara na huduma wanazotoa.