Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Prof.  Kahyarara awahimiza wafanyabiashara Mkoa wa Geita kuchangamkia fursa ya biashara na uwekezaji hasa katika utoaji huduma ya kulala wageni


Prof.  Kahyarara awahimiza wafanyabiashara Mkoa wa Geita kuchangamkia fursa ya biashara na uwekezaji hasa katika utoaji huduma ya kulala wageni

Katibu Tawala Mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara amewahimiza wafanyabiashara wa Mkoa wa Geita kuchangamkia fursa ya ufanyaji biashara ya huduma hasa katika ujenzi wa hoteli kwa ajili ya kulala wageni.

Prof. Kahyarara ameyasema hayo tarehe 20 Julai, 2023 wakati wa mafunzo kwa wadau wa sekta ya umma na binafsi mkoani Geita.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini (MKUMBI) ambao ni utekelezaji wa mradi wa Business Environment Growth and Innovation (BEGIN) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Prof. Kahyarara ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetengeneza mazingira mazuri na wezeshi ya ufanyaji biashara nchini hasa kwa kufuta tozo, ada na  marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia wawekezaji wengi zaidi iliyopelekea kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi.

Naye mwakilishi wa wafanyabiashara Mkoa wa Geita Mhandisi Chacha Mwita Wambura amesema kuwa mafunzo hayo kwa wafanyabiashara yamekuja kipindi kizuri ambapo wafanyabiashara wanahitaji kupata elimu ya taratibu nzuri za ufanyaji biashara hasa biashara za kimataifa ili kukidhi vigezo vya kuuza nje ya nchi na kuyafikia masoko ya kikanda na kimataifa.

Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Mtangamano wa Biashara Bi. Aneth simwela amesema kuwa wizara imetoa mafunzo hayo katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Mwanza, Geita na baadaye mikoa mingine itafuata.

Bi. Aneth ameongeza kuwa elimu inayotolewa ni juu ya taratibu za ufanyaji biashara mipakani, fursa za biashara katika masoko ya kikanda (EAC, AfCFTA, SADC, Biashara baina ya nchi na nchi, vikwazo vya biashara visivyokuwa vya kiushuru (NTBs), vigezo vya viwango vya afya ya wanyama, mimea na usalama wa chakula katika ufanyaji biashara (sanitary and phytosanitary measures  SPS), masuala ya vikwazo vya biashara vya kiufundi, Uelewa kuhusu mkataba wa uwezeshaji biashara wa shirika la Dunia (WTO) na masuala ya biashara ya mtandao.