Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

PROF. MKUMBO AWATAKA TBS KUWEKA MPANGO WA KUWAPATIA ELIMU NA NEMBO ZA UBORA WAJASIRIAMALI NA WAFANYABISHARA WADOGO .


Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuweka mpango maalum wa kusaidia Wajasiriamali wadogo na Wafanyabiashara ndogo na za kati (SMEs) ili kuwainua kwa kuwapatia elimu ya uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi viwango na  kuwapatia nembo za ubora.

 

Prof. Mkumbo ameyasema hayo katika hafla ya utoaji wa tuzo  za ubora kwa washindi wa mwaka 2020 na ufunguzi wa mashindano ya tuzo za kitaifa za ubora kwa mwaka 2021 iliyofanyika makao makuu ya TBS , Ubungo Dar es salaam. Novemba 15, 2021

 

“TBS muweke na mpango maalum wa kuwafundisha, kuwaelimisha Wajasiriamali wadogo na Wafanyabiashara ndogo (SMEs)  wajue namna ya kuzalisha bidhaa bora na namna ya kupata nembo ya ubora, punguzeni urasimu wa kuwatambua na kuwapa idhibati” amesema Prof. Kitila Mkumbo

 

Prof. Mkumbo amesema kuwa kufuatia makubaliano baina ya wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) tuzo za ubora zilianzishwa ili kutambua na kukuza sekta ya biashara kupitia ubora na bidhaa na huduma katika ukanda huu.

 

Amesema tuzo hizi ni sehemu ya mipango ya Serikali kuendelea kuboresha huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini katika kuhakikisha kuwa huduma na bidhaa zinakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa na kuweza kuhumili soko la ushindani kidunia.

 

Aidha, Prof. Mkumbo amebainisha kuwa tuzo zipo katika maeneo makuu mawili ambayo ni washiriki wadogo na wa kati na washiriki wakubwa vilevile zipo katika makundi makubwa matano ambayo ni Kampuni bora ya mwaka, bidhaa bora ya mwaka, huduma bora ya mwaka, muuzaji bora wa bidhaa nje na tuzo binafsi kwa mtu aliyechangia katika kuendeleza viwango vya ubora katika SADC.

 

Wakati huo huo, Prof. Mkumbo ametoa tuzo kwa washindi wa mashindano ya tuzo za ubora kwa mwaka 2020 ambao ni mshindi wa Kampuni bora ya mwaka ni  Geared Consulting Engineering, Mshindi wa bidhaa bora ya mwaka ni Zanzibar Milling corporation Ltd na Lilian Production Group na Mshindi binafsi aliyechangia katika kuendeleza viwango vya ubora katika SADC ni Kezia Mbwambo.

 

Vilevile, Prof. Mkumbo amemetoa wito kwa makampuni na wadau wote kushiriki kwenye tuzo hizo hususani wale ambao hawakuwahi kushiriki ili nchi yetu iweze kupata wawakilishi katika mashindano ya tuzo kwenye Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za kusini mwa Afrika (SADC).

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania, Dkt. Athuman Ngenya ameeleza kuwa malengo ya kuanzisha tuzo hizo ni pamoja na kuwatambua na kuwapongeza watu binafsi pamoja na taasisi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya ubora wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za uzalishaji bidhaa na utoaji huduma.