Habari
Wataalamu wa sekta ya biashara kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakishughulikia changamoto za wananchi
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo (Mb) ametoa wito kwa wataalamu wa sekta ya biashara kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakishughulikia changamoto za wananchi kwa umakini na kutoa taarifa sahihi.
Dkt. Jafo ameyasema hayo Mei 5, 2025, wakati wa ziara yake katika Soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambapo alikutana na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko hilo.
DKt. Jafo ameagiza wataalamu wote wa masuala ya biashara pamoja na vyombo husika kuendelea na ukaguzi wa wafanyabiashara wasiokuwa halali katika Soko la Kariakoo kuanzia Mei 6, 2025 na kueleza kuwa ukaguzi huo ni muhimu kwa sababu bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wafanyabiashara wazawa wanapata haki zao ipasavyo.
Aidha, Waziri Jafo amesema serikali inaendelea na maboresho ya sheria ili kubainisha kwa uwazi aina za biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, na zile ambazo wageni wanaruhusiwa kuzifanya kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko hil na kusisitiza kuwa maboresho hayo yanafanyika kwa ushirikiano na wafanyabiashara ili kuhakikisha sheria hizo zinaendana na mazingira halisi ya biashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Edward Mpogolo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema wataendelea kuhakikisha Soko la Kariakoo linabaki salama kwa ajili ya shughuli za kibiashara, ili wafanyabiashara waendelee kunufaika na biashara zao na kuahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa wafanyabiashara kuhakikisha wanapata faida stahiki kutokana na biashara zao.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuagiza Waziri Jafo kufuatilia kwa karibu operesheni ya duka kwa duka ili kubaini wafanyabiashara wanaofanya biashara kinyume na taratibu.
Mjumbe wa Kamati, Hamis Lumembe, amepongeza hatua za serikali kupitia na kujiridhisha kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kuhusu uwepo wa wafanyabiashara wageni wengi wanaofanya biashara bila vibali halali.