Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kiwanda cha kuunda magari cha Saturn Corporation Limited kuendelea kushirikiana na wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt,Selemani Jafo ( Mb) amewasihi wadau wa kiwanda cha kuunda magari cha Saturn Corporation Limited kuendelea kushirikiana na wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini.

Dkt.Jafo amasema hayo katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa kiwanda hicho kilichopo Kisarawe 2, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam Mei 11,2025.

Aidha Dkt.Jafo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicholaus Shombe kuhakikisha kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre kinafufuliwa na kuendelea kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza nchini ili kuongeza ajira za vijana.

Waziri Jafo ameongeza kuwa ni furaha kuona teknolojia ya utengenezaji wa magari hasa malori makubwa ikifanyika hapa nchini hivyo amekipongeza kiwanda cha Saturn kwa kuendelea kusimamia malengo ya kuzalisha magari, pamoja na kwenda na ajenda ya viwanda inayosema hadi kufikia mwaka 2030, nchi inatarajiwa kuwa ya viwanda zaidi ambayo itasaidia kuchochea ajira kwa vijana.

Hata hivyo, alikipongeza kiwanda hicho kwa kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi wake ni vijana hivyo ametoa rai kwa vijana hao kuhakisha wanafanya kazi kwa bidii na ubora zaidi.

Pia Dkt.Jafo ametoa rai kwa wadau mbalimbali hususani katika viwanda, kuhakikisha wanatumia fursa kununua magari hayo katika kiwanda cha Saturn ambacho kinazalisha vitu vya mdani.

Nae Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha kuunganisha malori na matipa, Rehamatullah Habib, ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wanaowapa, huku akibainisha kuwa hata uzalishaji wa katika kiwanda hicho umeongezeka. Kwani hapo awali kilikuwa kinaunganisha magari matatu, hivi sasa magari 12 yanaunganishwa kwa awamu moja.