Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali haitambui kuwa Gunia ni Kipimo - Mhe-Kigahe


Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe amesema kuwa Serikali haitambui kuwa Gunia ni kipimo bali itambulike kuwa ni Kifungashio kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo (The Weights and Measures Act (Amendment) Order, G.N. No. 725 of 2018,) jedwali la 10 chini ya kifungu cha (2) (b) cha Jedwali hilo, ambacho kinasema mazao ya mashambani yatafungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu 100.

 Mhe.Kigahe ameyasema hayo Septemba 6,2023 Bungeni Jijini Dodoma alipojibu swali la Mhe. Husna Sekiboko lililolenga kutaka kujua kama kwa mujibu wa Sheria Serikali inatambua gunia kuwa kipimo au kifungashio.

Aidha Naibu Waziri Kigahe ametoa wito kwa wadau wote kuepuka matumizi ya gunia kama kipimo kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria ya Vipimo.

Vilevile Mhe. Kigahe amewataka wakulima wa mazao ya mashambani kuendelea kujiunga kwenye vyama vya msingi pamoja na kuuza mazao yao kwenye masoko ambayo Serikali imeelekeza Wakala wa Vipimo kupeleka Mizani kwa ajili ya upimaji wa mazao hayo