Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wajasiriamali kupata fursa ya kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.


Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wajasiriamali kupata fursa ya kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Kigahe ameyasema hayo Machi 11, 2023 katika hafla ya utoaji tuzo za Wanawake wanaozalisha bidhaa za Viwandani  zilizoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Biashara Wanawake Tanzania (TWCC) iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani city Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo TWCC imekuwa ikitambua bidhaa zinazo zalishwa  na Wajasiriamali hapa nchini na kwamba kwa kupitia majukwaa yao kumekuwa na fursa  nyingi zinazolenga kuwasaidia Wajasiriamali hao kufikisha bidhaa zao kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha ameipongeza TWCC kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwawezesha na kuwainua Wanawake wafanyabiashara kote nchini.

“Ni wazi kuwa Mwanamke akiwezeshwa katika Biashara uchumi wake utaimarika na ataweza kuisaidia familia yake na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla” amesema Mhe. Kigahe 

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa TWCC Taifa Bi.Mercy Silla amesema kuwa Tuzo hizo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambapo kila mwaka TWCC inasherehekea siku hiyo kwa kuandaa maonesho ya Wajasiriamali kuonesha bidhaa zao wanazozalisha na kuhitimisha kwa hafla kubwa ya utoaji tuzo kwa Wajasiriamali wao.

Sherehe hizo za utoaji tuzo kwa Wajasiriamali ziliudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Umma, pamoja na Sekta Binafsi, ambapo jumla ya tuzo 70 zilitolewa.