Habari
SERIKALI IMEHAMASISHA MASHIRIKA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI NCHINI KUCHANGAMKIA FURSA ZILIZOPO KWENYE MAONESHO YA EXPO 2020 DUBAI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyahamashisha Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi hapa nchini kuendelea kujitokeza katika kushiriki Maonesho Makubwa ya Dunia ya Expo 2020 Dubai yanayofanyika kuanzia tarehe 1 Oktaba, 2021 hadi 31 Machi, 2022 Umoja nchi za Falme za Kiarabu (UAE), ili waweze kuzitumia fursa zinazopatika kwenye Maonesho hayo za Utalii, Madini, masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa hapa nchini pamoja na kupata wabia wa biashara.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Dotto James katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliowashirikisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Bianafsi (TPSF) Bw. Francis Nanai na Mtendaji Mkuu wa Balaza la Biashara la Taifa (TNBC) Dkt. Godwill Wanga uliofanyika leo tarehe 26 Oktoba, 2021 Jiji Dar es Salaam.
Bw.Dotto James ametoa wito kwa makampuni yanayojushughulisha na biashara ya Madini, Utalii, Nishati, Ujenzi, viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na wengine waweze kujitokeza kushiriki katika banda la Tanzania kulingana na ratiba, makongamano na ziara za kibiashara kupitia programu zilizoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Ameongeza kuwa hadi sasa, Ushiriki umehusisha Sekta za Umma zaidi, hivyo ametoa wito kwa Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu.
” Tunaamini tukiitumia vema fursa hii tutapata masoko endelevu ya bidhaa zetu, wabia wa uhakika na zaidi tutapata elimu na uzoefu kutoka kwa wenzetu “ Alisema Bw.Dotto James
Aidha, amesisitiza ushiriki wa Sekta ya Utalii kwa ujumla kwakuwa una nafasi kubwa katika ushiriki huu kwa sababu Tanzania ina vivutio mbalimbali vya kipekee kama vile Mbuga za Wanyama, fukwe za bahari, na maeneo ya kihistoria yanayoweza kuyatangazwa kimataifa ili kupata wawekezaji wakubwa na watalii wengi zaidi hasa kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE).
“ wadau wa Sekta ya Madini wanatakiwa kuchangamkia fursa hii kupata wawekezaji na wabia wa biashara ya madini hasa katika madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee. Alisema Bw. Dotto James
Pia amewataka Wakuu wa Taasisi ambazo ziinashiriki kuweka namna nzuri ya kuitangaza nchi kupitia sekta zao ikiwemo miradi ya kuvutia wawekezaji katika ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na taasisi za TRC, TPA, TANROAD, TTCL, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), TANESCO na miradi yenye fursa za uwekezaji kutoka taasisi nyingine za umma na binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Bianafsi (TPSF) Bw. Francis Nanai alitumia fursa hiyo kuwataka wadau wote wa sekta za biashara nchini kutumia maonesho haya katika kujitangaza, kutafuta masoko nje ya nchi na hata kujifunza kutoka kwa wengine namna ya ufanyaji biashara . ‘Mimi nimetoka kule, nimeona fursa nyingi sana kuanzia masoko na wabia wa bishara katika sekta nyingi, tuitendee haki nchi yetu, Dubai ni karibu sana’’ aliongeza Bw.Nanai
Naye Mtendaji Mkuu wa Balaza la Biashara la Taifa (TNBC) Dkt. Godwill Wanga alisema kuwa Maonesho hayo ni muhimu sana kwa Taifa letu kwani ni nafasi ya kupanua Diplomasia ya uchumi wa dunia kwani dunia nzima inakutana Pamoja hivyo ni nafasi ya kujifunza biashara lakini hata pia tamaduni jambo ambalo ni muhimu katika kupanua wigo wa biashara ikiwa ni Pamoja na kujifunza namna ya ufanyaji biashara kidigitali.