Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

VIWANDA NGUO VYAHIMIZWA KUTUMIA LEBO YA “MADE IN TANZANIA”


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesisitiza viwanda vinavyozalisha na kuchakata nguo nchini kuweka lebo ya “Made in Tanzania” katika nguo hizo ili kuendelea kujitangaza kimataifa na kutambulisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kapinga ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Machi 2026 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha nguo cha Sunflag (Tanzania) Limited, Bw. Emmanuel Mwabuka.

Katika mazungumzo hayo, walijadili mipango ya kuviwezesha viwanda pamoja na changamoto mbalimbali vinazokabiliana nazo, na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kuendelea kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Aidha, pande hizo mbili zilijadiliana kuhusu namna bora ya kuhakikisha viwanda vya nguo vinapata malighafi ya pamba kwa uhakika, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuwawezesha wakulima wa pamba na kuongeza thamani ya zao hilo hapa nchini.