Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali imesema kuwa itahakikisha inaongeza ufanyaji biashara na nchi ya India pamoja na bara la Asia kwa ujumla katika kilimo, teknolojia viwanda na elimu.


Serikali imesema kuwa itahakikisha inaongeza ufanyaji biashara na nchi ya India pamoja na bara la Asia kwa ujumla katika kilimo, teknolojia viwanda na elimu. 

Hayo yamesemwa Julai 7, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban katika kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka India na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) waliofika na kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kushiriki na kuhudhuria katika maonesho ya 47 ya kimataifa ya biashara Maarufu (Sabasaba) yanayoendelea.

Waziri Omar ameongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya sera za uwekezaji na elimu hususani eneo la teknolojia nchini hasa kufuatia kuanzishwa kwa Kampasi ya chuo Kikuu cha Teknolojia cha Indian Institutes of Techology (IITs) Mjini Zanzibar kitasaidiay kuimarisha teknolojia na uzalishaji wa bidhaa kwa njia za kisasa na kuongeza ufanisi katika shughuli za uzalishaji viwandani, huku akitanabaisha kuwa mazao ya kilimo yataongezeka maradufu katika kuzalishwa na kusafirishwa kuelekea nchini India.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Gilead Teri amesema kuwa kutokana na mabadiliko mbalimbali ya sera za biashara, kumaimarika kwa ufanyaji biashara, na uwekezaji yanayofanywa na serikali yamezidi kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza nchini, hivyo jambo hilo linazidi kuongeza fursa za biashara na uwekezaji na kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na kutoa wito kwa wawekezaji kuendelea kuja kuwekeza hapa nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya India S. Jaishankar aliyeambatana na ujumbe wake amesema kuwa Tanzania na India wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo, maji, afya, teknolojia, elimu, uwekezaji, diplomasia hivyo nchi hiyo itaendelea kuhakikisha ushirikiano huo unaendelea kukua na kuelta manufaa zaidi kwa nchi zote.

Kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuwatambulisha wafanyabiashara hao katika maeneo ya uwekezaji hapa nchini ingawa imeelezwa kuwa wawekezaji waliokuja watarajie kuwekeza zaidi kwenye maeneo ya uchakataji wa chakula (Food processing), bidhaa za misitu, (Wood products) lakini pia bidhaa za ujenzi kama vile nondo, saruji, chuma, sekta ya elimu, afya na viuatilifu na bidhaa za chanjo.