Habari
Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ongezeko la bei ya mchele

Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ongezeko la bei ya mchele ikiwa ni pamoja na kutoa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje ya nchi ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2023 jumla ya tani 90,000 za mchele zinatarajiwa kuingia sokoni na hivyo kushusha bei ya bidhaa hiyo.
Hii ni kutokana na kuelekea kuanza kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma, ambapo lengo la Serikali ni kuhakikisha bei ya bidhaa zote zinazotumika kwa wingi kwenye kipindi hiko hazipandi.
Hayo ameyasema leo jijini Dar Es Salaam, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Februari 2023 ambapo alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kwenye maeneo yote ambayo yanaonekana kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ili waendelee kubaki kwenye wigo wa mfumuko wa bei waliokubaliana ndani ya Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
"Tunaelekea kuanza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma, ni matarajio ya Serikali kwamba bei ya bidhaa zote zinazotumika kwa wingi kwenye kipindi hiki hazitopanda. Ndugu zangu Wazalishaji wa sukari, tumekuwa na vikao vya pamoja na kwa umoja wetu tumekubaliana tuna sukari ya kutosha ndani ya nchi yetu hivyo hatutarajii kuona bei ya sukari inapanda"
"Bei ya Unga wa ngano imeonyesha kushuka ndani ya miezi hii miwili, hivyo hatutarajii kuona ikipanda tena kwani Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwa na bidhaa hii ya kutosha ndani ya nchi yetu."
Pia alisema yapo maeneo ndani ya Nchi ya Tanzania wameanza kuvuna maharage hivyo hawatarajii kuona bei ya bidhaa hiyo muhimu ikipanda tena.
"Bei ya maharage kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 2,300 na 4,000 kwa kilo. Bei ya chini imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 2,400 kwa kilo. Bei ya chini inapatikana katika Mkoa wa Songwe na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Shinyanga."
Aidha Dkt. kijaji aliwataka wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeza jitihada za uzalishaji wa bidhaa na kwa ubora unaohitajika sokoni kwani kumekuwepo na malalamiko ya watuamiaji wa bidhaa za viwandani kuhusu ujazo na hata ubora wa bidhaa hizo.
Hivyo aliwataka mawakala wa Vipimo Tanzania kufanya Ufuatiliaji wa karibu juu ya malalamiko hayo na hatua madhubuti zichukuliwe kwa wote Watakaopatikana na kosa la kuzalisha bidhaa chini ya kiwango na ujazo unaohitajika na ulioonyeshwa kwenye vifungashio.
Kuhusu Bei za vifaa vya ujenzi kwa mwaka 2023, Dkt. Kijaji alisema zimeendelea kushuka kutokana na kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa bidhaa hizo sambamba na usimamizi madhubuti wa mwenendo wa soko la bidhaa hizo uliofanywa na Wizara na taasisi zake.
"Bei ya saruji kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 14,750 na 23,500 kwa mfuko wa kilo 50. Bei hiyo imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023. Mikoa yenye bei ya chini ni Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Pwani na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Mara, Kigoma na Katavi."
"Bei ya nondo mm 10 kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 16,100 na 25,000. Bei ya chini imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 17,500. Bei ya juu ya nondo mm 10 imepanda ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 23,000. Bei za chini zipo katika Mikoa ya Kilimanjaro, Iringa, Mwanza na Tanga na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Lindi."
Kwa upande wa Bei ya Bati, Dkt. Kijaji alisema,
bei ya bati nyeupe geji 30 kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 22,000 na 30,000, Bei ya chini ya bati imepungua ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari, 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 22,500.
"Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Tanga, Songwe,Kilimanjaro Singida na Ruvuma na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Njombe."
Dkt. Kijaji alisema Bei ya Sabuni aina ya Jamaa, White wash na MO kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 2,500 na 4,000 kwa mche ambapo bei ya chini ipo katika Mkoa wa Simiyu na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Mbeya.
Bei ya Sabuni aina ya Takasa, kiboko na Kuku kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 1,200 na 3,250 kwa mche huku bei ya chini ipo katika Mkoa wa Mara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Ruvuma na Tanga.
Kwa bei ya Sabuni za Magadi kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 1,000 na 3,250.
" Sabuni za magadi zipo aina mbili nazo ni miche myembamba na miche minene. Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Dodoma na Mara."
Kwa Bei ya Viazi Mviringo Dkt. Kijaji alisema kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 1,000 na 1,750 kwa kilo. Bei ya chini imepanda ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 800 kwa kilo, Bei ya juu ya Viazi Mviringo imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 2,000. Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Songwe,Tanga na Mbeya na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Manyara, Mara na Ruvuma.
Aidha Dkt. Kijaji alisema bei ya mafuta ya kupikia ya Alizeti kwa mwezi Februari ni kati ya Shilingi 4,750 na 7,800 kwa lita. Vile vile, bei ya mafuta ya kupikia ya Mawese (Korie na Safi) ni kati ya Shilingi 4,500 na 7,250 kwa lita.
"Bei ya mafuta ya kupikia imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Januari, 2023. Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya Alizeti ipo katika Mikoa ya Manyara, Morogoro na Singida na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Mara."