Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali inatambua juhudi za sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika viwanda vya kukamua mbegu za mafuta.


Hayo yamesemwa leo tarehe 17 Agosti,2023  na  Mhandisi  Wilson Lugano, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Viwanda aliyemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara katika hafla  ya kuzindua mtambo wa kusafisha mafuta ya Alizeti katika kiwanda cha Quickstep Investment LTD kilichopo Mkoka, Wilaya ya Kongwa, Dodoma.

Mhandisi Lugano amesema mtambo huo umesanifiwa na kutengezwa na wataalam Wakitanzania ambao wanatoka VETA hivyo ni mali ya watanzania wenyewe pia ni hatua muhimu katika uchumi wa viwanda.

Ameishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa na Maendeleo ya Viwanda UNIDO kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha inaendelea kusaidia sekta ndogo ya mafuta ya kula nchini.

Naye Mwakilishi wa UNIDO, Gerald Runyoro amesema Shirika hilo limefadhili mitambo mitatu na mmoja wapo ndio umetolewa katika kiwanda cha Quickstep Investment LTD ambacho kilikidhi vigezo vilivyotolewa. “Tunajua wazalishaji ni wengi, lakini hatuwezi kuwafadhili wote hivyo UNIDO kitu inachofanya ni kupitia katika taasisi za serikali au watu binafsi waliokidhi vigezo ambazo wanafanya kazi moja kwa moja na wazalishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali kwa mfano SIDO, VETA, TBS, na TIRDO”.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA  Anthony Kasore  amesema dhamira ya kubuni mtambo huo  ni  kuhakikisha wajasiliamali na wazalishaji wa mafuta wakuwa na mafuta yenye ubora na viwango vinavyohitajika katika soko la ndani ya nchini na nje. Alibainisha kuwa mtambo huo umegharibu shilingi milioni 17.9 hadi kukamilika.

Kwa upande wake Meneja wa SIDO Dodoma Bw. Twaha Swed ameishukuru UNIDO kwa kutoa teknolojia hiyo ya kusafisha mafuta, na amehaidi kutoa elimu kwa wajasiliamli  namna bora ya kuchakata mafuta ili waweze kuzalisha kwa tija na kuleta manufaa katika soko la mafuta ya alizeti nchini.  

Naye mwenyekiti wa Wasindikaji mafuta Bw. Ringo Iringo ametoa wito wa kusimikwa mitambo hiyo katika sehemu mbalimbali nchini ili wazalishaji waweze  kusafisha mafuta kupitia mitambo hiyo, aliongeza kuwa soko la mafuta double refined lipo ila wazalishaji wengi wanajua kusafisha mafuta mara mbili au tatu ndio double refined, lakini kuna utaratibu wake.