Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali itaendelea kuliwezesha Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuboresha Mfumo wa uendeshaji na utoaji wa huduma bora na wezeshi zinazotumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Prof. Kahyarara ameyasema hayo wakati wa utoaji wa taarifa ya utendaji ya SIDO kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu utekelezaji wa majukumu ya SIDO na mafanikio yake iliyofanyika Februari 4, 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, Kutokana na umuhimu wa SIDO nchini, Kamati hiyo imeliagiza Shirika hilo kuongeza juhudi katika kuwezesha watanzania kuanzisha Viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha bidhaa muhimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mahitaji ya soko ili kupunguza utegemezi na uagizaji wa bidhaa hizo nje ya nchi, pia kuongeza ajira na pato la Taifa.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji wa Shirika hilo kwa Kamati hiyo, Mkurugenzi wa SIDO Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji alieleza kuwa SIDO imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia, Uanzishaji wa miradi ya viwanda vidogo vijijini, Mafunzo, Ushauri na huduma za ugani, Masoko na Habari, na Huduma za fedha kwa wajasiliamali wadogo.
Aidha, Amesema SIDO imeendelea kujenga mabanda (Industrial shades) katika kila mkoa yanayowawezesha wajasiliamali kuanzisha viwanda katika maeneo hayo kwa urahisi ambapo hadi sasa Shirika lina Mitaa ya Viwanda katika Mikoa 21 ambayo ina Majengo ya Viwanda 673. yanatumiwa na Viwanda 573 yenye ajira 5,297.

Pia, amesema SIDO imejipanga kutanua uwigo wa utuoaji huduma inayopatikana katika mikoa yote na kuelekeza huduma hizo katika kila wilaya ili kuongeza kasi ya uanzishaji na ukuzaji wa viwanda vidogo nchini ambavyo vitaongeza ajira na kukuza biashara na uchumi wa nchi.