Habari
Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yenye ushindani.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yenye ushindani, endelevu,na yatayovutia wawekezaji zaidi kuja nchini.
Aliyasema hayo tarehe 23 Februari, 2023 katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya lililofanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2023 JNICC, Dar es Salaam.
Bwana Gugu aliongeza kuwa kuongezeka kwa uwekezaji nchini kutainufaisha Tanzania kwa kutengeneza ajira nyingi ifikapo mwaka 2025 na pia kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa.
Akielezea Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) nchini amesema maboresho mengi yamefanyika ikiwemo kufuta tozo, ada na faini 232, kuoanisha taasisi kwa wale waliokuwa na majukumu yanayoingiliana, kuanzishwa kwa Mfumo wa Dirisha Moja la Kielektroniki litakalokuwa likitoa huduma kupitia njia ya mtandao.
Alilisisitiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ina majukumu kadhaa ambayo yanalenga kuhakikisha utimilifu wa kukuza wigo wa tasnia yenye ushindani na endelevu yenye msingi wa kimataifa wa biashara kupitia sera, mikakati na mipango ya mageuzi jumuishi ya viwanda.
Aidha, aliongeza taasisi zilizo chini ya Wizara zina majukumu maalum katika kuendeleza sekta ya uwekezaji viwanda na biashara nchini.