Habari
Serikali kuendelea kuhamasisha uwekezaji na uendelezaji wa viwanda Nchini-Mhe.Kigahe

Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe Exaud Kigahe amesema kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vipya na uendelezaji wa viwanda vilivyopo katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi hususani Viwanda vya kuchakata mazao ya Mifugo na Uvuvi vikiwemo viwanda vya Nyama na Samaki katika Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine nchini.
Mhe.Kigahe amebainisha hayo Septemba 8,2023 Bungeni Jijini Dodoma alipojibu swali la Mhe. Bupe Nelson Mwakang’ata linalotaka kufahamu kuwa ni lini Serikali itaviendeleza viwanda vya nyama na samaki mkoani Rukwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka nguvu kubwa katika unenepeshaji wa mifugo pamoja na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, kutenga na kuboresha maeneo ya kukusanyia samaki (collection Centers) pamoja na minada ya mifugo ili kukidhi haja ya upatikanaji endelevu wa malighafi bora ya viwanda vya nyama na samaki nchini.
Vilevile Mhe.Kigahe ametoa rai kwa wavuvi na wafugaji kuviuzia malighafi viwanda vya ndani ili viweze kukidhi mahitaji yake.