Habari
Serikali kuendelea kuwafikia Wafanyabiashara
Serikali kuendelea kuwafikia Wafanyabiashara, kuwasikiliza hoja za Kibiashara na kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kuweka mazingira mazuri ya Kibiashara*
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe ( Mb) ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kuchangia pato la Taifa kwa kulipa kodi kwa hiari.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo Septemba 14, 2024 wakati akijibu hoja za wafanyabiashara wa Ngara katika Mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari ya Ngara.
Katika kiko hicho, Wafanyabiashara hao wamewasilisha hoja mbalimbali ikiwemo utitiri wa Biashara za magendo na zisizo fuata utaratibu zinazoingia nchini Tanzania kutoka nchi jiarani na kuuzwa nchini kwa bei nafuu tofauti na bidhaa za hapa nchini zinalipiwa kodi na kuingizwa kwa njia rasmi.
"Ndugu zangu niwaombe sana sisi kama Serikali tumesikikiza hoja zenu, zile zinazowezekana tutazifanyia kazi, pia nanyi mtimize wajibu wenu kwa kulipa kodi. Mnapolipa kodi bila shuruti mnaiongezea Serikali pato ambalo litasaidia kuteleleza miradi ya Maendeleo na kuinua uchumi wa nchi "Amesema Kigahe.
Ameongeza kwa kusema kuwa licha ya kupoteza mapato ya Taifa pia wananchi wanapata madhara ya kiafya kwa kula vyakula ambavyo vinaingizwa hapa nchini kinyemela bila kuwa na ubora wa TBS
Aidha, Mbunge wa jimbo la Ngara Mhe. Ndaisaba Ruhoro ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biasha kwa kufika katika Wilaya ya Ngara kujibu na kutolea ufafanuzi mzuri juu ya hoja za Wafanyabiashara.
"...Wananchi wa Ngara wanapata changamoto z Kibiashara kupitia Mipaka ya Kabanga na Rusumo. Mipaka hii ni mikubwa na Biashara za magendo zinaadhiri biashara za wananchi wetu". Amesema Mhe. Ndaisaba Ruhoro.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wilaya ya Ngara Bw. Chrispine Kamugisha amemweleza Naibu waziri wa Viwanda na Biashara kuwa changamoto za mipakani ni endelevu kwasababu ya mifumo inabadilika mara kwa mara ambapo hupelekea wafanyabiashara kufilisika.
"Wafanyabiashara wanapofilisika huwa wanakuja wengine wapya kufanya Biashara hivyo tunaomba Wizara kuwa na zoezi endelevu la kutoe Elimu kwa wafanya Biashara wapya `` Amesema Kamugisha.