Habari
Serikali kufanya Sensa ya uzalishaji Viwandani kwa mwaka wa Rejea 2023(Census of Industrial Production 2023) mwezi machi 2025.
Serikali kufanya Sensa ya uzalishaji Viwandani kwa mwaka wa Rejea 2023(Census of Industrial Production 2023) mwezi machi 2025.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) wakati akizungumza na waandishi wa habari Februari 4, 2025 katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Jafo amesema kuwa Sensa ya uzalishaji Viwandani ya mwaka wa Rejea 2023 itakuwa ya kwanza kufanyika katika pande zote mbili za Muungano wa Jamhuri ya Tanzania tangu mwaka 1964.
Aidha, suala la takwimu ni miongoni mwa mambo ya Muungano (namba 20 kwenye orodha ya mambo ya Muungano) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,Tanzania bara ilifanya Sensa za uzalishaji Viwandani mwaka 1963,1978,1989 na 2013 na Kwa upande wa Zanzibar zilifanyika mwaka 1989,2002,2008 na 2012.
Vilevile taarifa za viwanda zitakazokusanywa zitahusisha shughuli za kiuchumi zilizofanyika katika viwanda ambapo shughuli zitakazojumuishwa ni pamoja na utengenezaji wa bidhaa za viwanda,uchimbaji wa madini na kokoto, uzalishaji na usambazaji wa umeme,gesi,mvuke na kubadilisha hali joto au baridi na usambazaji wa maji safi,mifumo ya kukusanya maji taka,udhibiti wa taka na shughuli za urejeshaji(recycling).
Pia amesema Sensa ya uzalishaji Viwandani ya mwaka 2023 itakusanya taarifa kutoka viwanda vyote ambavyo vimegawanywa katika makundi mawili makuu ambapo Kuna kundi la viwanda vyenye wafanyakazi kuanzia kumi au zaidi na kundi la viwanda vyenye wafanyakazi kuanzia mmoja hadi tisa.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt.Albina Chuwa alisema kuwa Sensa hiyo ya uzalishaji viwanda itafanyika kwa miezi mitatu,yaani Mwezi Machi,Aprili na Mei ambapo Mwezi Juni, 2025 wanatoa matokeo na kuelezea wananchi mafanikio makubwa ndani ya Sekta ya Viwanda ambayo inachukua taswira kubwa katika nchi yetu.