Habari
Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwanyanyua wanawake wajasiriamali nchini

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwanyanyua wanawake wajasiriamali nchini kwa kuhakikisha wanapata elimu ya ujasiliamali na kuendeleza mawazo yao ya kibiashara.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kufunga mafunzo ya wajasiriamali yaliyofanyika Juni 6, 2022 jijini Dodoma amesema ni wajibu wa wanawake kuchangamkia fursa hizo.
Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wanawake (Academy of Women Entrepreneurs – AWE) Tanzania Dkt. Victoria Kisyombe pamoja na wanufaika 31 wa mafunzo hayo maalum ya wiki 10 wameeleza namna mafunzo hayo yanavyosaidia kukuza ujasiriamali nchini.
Naye, Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Donald Wright amesema Serikali ya Marekani imeongeza dola laki moja za ziada kufadhili mafunzo kwa wanawake wajasiliamali kwa mikoa minne mwaka 2023 nchini Tanzania na kueleza matokeo ya mafunzo hayo.
“Mafunzo ya wiki 10 mliyoyapata mkiwa sehemu ya programu hii yamewapa ujuzi kwa vitendo utakaowawezesha kuanzisha biashara endelevu pamoja na kuwaunganisha na wakufunzi (mentors) na wajasiriamali kama ninyi wa nchini Marekani,” alisema.
Washindi wanne bora katika mafunzo hayo ya ujasiriamali yaliyotolewa jijini Dodoma kwa wiki kumi na tatu watapatiwa mtaji wa dola elfu kumi ili kuendeleza mawazo yao ya kibiashara.