Habari
SERIKALI YAHAIDI KUKAMILISHA NA KUTEKELEZA MKATABA WA MAKUBALIANO KATI YA KOSGEB YA UTURUKI NA SIDO YA TANZANIA.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amesema Serikali itakamilisha na kutekeleza Mkataba wa Makubaliano kati ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda vidogo na Biashara ndogo na za kati (KOSGEB) la Uturuki na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) la Tanzania kwa lengo la kuipatia SIDO mafunzo na uzoefu katika kuboresha utoaji msaada na uwezeshaji wa Viwanda na Biashara ndogo na za kati (SMEs).
Prof. Mkumbo amsema hayo alipotembelea KOSGEB akiwa
ameambatana na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar Bw. Omar Shaaban pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mazingira Mhe. David Makiposa, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Bw. Hassani Mwamweta na Maafisa wa Wizara ili kujifunza na kupata uzoefu wa jinsi ya kuboresha huduma zinazotolewa na SIDO ya Tanzania kwa SMEs.
Prof. Mkumbo na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea baadhi ya viwanda vidogo vinavyowezeshwa na KOSGEB na walifurahishwa na usimamizi na maendeleo ya viwanda hivyo katika utengenezaji ya bidhaa kwa kutumia ubunifu na teknolojia zinazokidhi mahitaji ya soko kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa KOSGEB Bw. Hassan Basri Kurt alimueleza Waziri Mkumbo na ujumbe wake kuwa Shirika hilo liko tayari kukamilisha Mkataba wa Makubaliano na SIDO ya Tanzania bara na kuanzisha Mkataba na Wakala wa Viwanda Vidogo vidogo, Vidogo na vya Kati (SMIDA) ya Zanzibar.
KOSGEB ina mikataba ya makubaliano 93 katika taasisi 88 katika nchi mbalimbali 69 pamoja na mashirika ya kimataifa matano (5), hivyo iko tayari kukamikisha makubaliano na SIDO ya Tanzania ambayo yako katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Akimueleza Waziri Mkumbo na ujumbe wake Kurt alisema KOSGEB imeanzishwa kwa ajili ya kutoa msaada muhimu na kuziwezesha kwa SMEs nchini humo na imejikita katika utafiti na maendeleo, uzalishaji wa teknolojia, bidhaa za nyumbani kwa ajiki ya mauzo ya nje, kuendeleza na kukuza ujasiliamali kimataifa
Kurt aliongeza kuwa SMEs nchini Uturuki ni asilimja 99 ya makampuni yote na huzalisha karibu asilimia 65 ya jumla ya uongezaji thamani katika sekta ya biashara na hivyo kufanya asilimia 73 ya jumla ya ajira katika biashara nchini humo.
Akieleza jinsi wanavyopata mapato ya kusimamia KOSGEB na kuziwezesha SMEs, alisema Shirika linapata fedha kutoka katika budget ya Serikali, ada kutoka makampuni yaliyowezeshwa na Shirika hilo, misaada au mikopo kutoka kwa wabia wa maendeleo.
Waziri Mkumbo na ujumbe wake wameshiriki Kongamano la tatu (3) la Uchumi na Biashara kati ya Uturuki na.Afrika lililoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki ikishirikiana na Wizara, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Kampuni ya Go Extra Mile Safaris na Benki ya CRDB iliyodhamini wafanyabiashara 100 kuhudhuria kongamano hilo kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu, kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania na kuimarisha ushirikiana kati ya wafanyabiashara wa Tanzaniana Uturuki.