Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Sheria Mpya ya Uwekezaji Ilenge Kuvutia Wawekezaji Ndani na Nje ya Nchi


Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ameeleza nia ya Serikali katika kuboresha Sheria ya Uwekezaji nchini ili iendane na matakwa ya sasa ya Uwekezaji wenye tija.

 Kigahe ameyasema hayo Oktoba 21, 2022 Bungeni Dodoma alipohudhuria kikao cha kupitia muswada wa Sheria ya Uwekezaji chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira.

 Kigahe ameieleza kamati hiyo kuwa kwa sasa nchi yetu inahitaji maendeleo ya kiuchumi hasa katika ukanda huu wa SADC ambapo kuna soko kubwa la kufanya Biashara baina ya nchi wanachama hivyo maboresho ya Sheria ya Uwekezaji nchini ni lazima ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza nchini ili kuongeza ajira kwa watanzania, kodi kwa Serikali na kukuza uchumi wa Nchi yetu.

 Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile (Mb) amesema kuwa Serikali imepanga kutengeneza mabilionea wengi zaidi hivyo basi ni muda muafaka sasa wa kufanyia kazi maboresho ya Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Nchini ili kuwalinda na kuwawezesha wawekezaji wa ndani waweze kuwekeza kwa kiasi kikubwa Nje ya Nchi na pia kuongeza idadi yawawekezaji kutoka Nje ya Nchi.

Aidha, Kihenzile ametoa pongezi kwa Mhe. Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ambaye amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa kamati yake katika hatua zote za majadiliano ya Muswada huo.

 Awali akiwasilisha taarifa ya Sheria zinazofanyiwa marekebisho katika Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 2022 Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji Bw. Aristides Mbwasi ameeleza baadhi ya vifungu vilivyojadiliwa na kamati na maoni yaliyotolewa ili kujadiliana maeneo yanayohitaji marekebisho katika kila sharia.